Na John Bukuku
SERIKALI
kupitia wizara zake nne tofauti zimeamua kufanya jitihada za kuondoa
changamoto ya msongamano wa wageni wanaiongia na kutoka nchini kupitia
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA) jijijini Dar es
Salaam.
Pia
kuondoa changamoto ya joto katika eneo la kuchukulia mizigo pamoja na
kushughulikia hati za kusafiria kwa wageni wanaoingia nchini pamoja na
changamoto ya ufinyu wa eneo la kusubiri huduma uwanjani.
Wizara
hizo zimekutana jana katika uwanja huo na kufanya ziara ya kukagua
shughuli za utoaji huduma kwa wageni na kubaini mambo kadhaa.
Mawaziri
hao ni Wizara ya Maliasili na Utalii Dk.Hamis Kigwangala, Wizara ya
Mambo ya Ndani Dk.Mwigulu Nchemba, Wizara ya Mambo ya Nje kupitia Naibu
Waziri Dk.Susan Kolimba na Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano
Atashasta Nditiye.
Akizungumza
uwanjani hapo baada ya kufanyika ziara hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya
Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Dk. Susan
Kolimba alisema wanaridhishwa na hatua zinazochukuliwa za kuondoa
changamoto zinazoelezwa kuwepo katika uwanja huo.
Alisema
baada ya kufanya ziara na kuona namna ambavyo huduma zinatolewa kwa
wageni mbalimbali wanaoingia nchini ameridhishwa na hatua ambazo
zinachukuliwa ni hakika zitaondoa kero hizo haraka.
“Awali mgeni alikuwa anahudumiwa kwa saa tatu lakini hivi saa mgeni anahudumiwa kwa saa moja,”alisema Dk.Kolimba.
Kwa
upande wa Waziri wa Mambo ya Ndani Dk.Mwigulu Nchemba alisema jitihada
zinafanywa kutatua changamoto hizo na kuna matumaini makubwa ya
kuzipatia ufumbuzi kwa haraka.
“Hatua
ambazo wizara yetu inachukua ni kuharakisha utoaji huduma wa hati ya
kusafiria kwa njia ya kieletroniki badala ya mfumo wa sasa na siku za
karibuni mchakato utakamilika.
“Pia
wizara yetu itaongeza idadi ya madawati ya kutolea huduma kwa wageni
ikiwa sambamba na kuongeza watoaji huduma uwanjani hapo,”alisema.
Alifafanua
kuwa taarifa zinaonesha kwa sasa kuna unafuu mkubwa wa kutoa huduma
kwani badala ya saa tatu ambazo zilikuwa zinatumia awali hivi sasa muda
wa utoaji huduma umeshuka hadi saa moja.
“Mbali
ya kuboresha huduma kwa nafasi yetu tutahakikisha pia tunaongeza ulinzi
na usalama katika viwanja vyetu vyote nchini ili kudhibiti wageni wenye
nia ovu na nchi yetu,”alisema.
Akizungumza
changamoto zilizopo uwanjani hapo Waziri wa Maliasili na Utalii
Dk.Kigwangala alisema wamefikia hatua hiyo baada ya baadhi ya wageni na
hasa watalii wanaiongia nchini kulalamika.
Alitaja
baadhi ya malalamiko ni kwamba wanatumia zaidi ya saa tatu kupata
huduma wakiwa uwanjani hapo.Pia joto kali na ufinyu wa eneo katika eneo
ambalo wageni wanasubiri kuhudumiwa.
Hivyo
Dkt.Kigwangala alisema kutokana na malalamiko hayo na mengine kadhaa
hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa na kueleza Agosti 8 mwaka 2017
manaibu waziri wa wizara hizo nne walikutana kwa ajili ya kutafuta
ufumbuzi.
Alisisitiza
ukarimu kwa wageni ni muhimu katika maeneo mbalimbali ya utoaji huduma,
akitoa mfano kuwa hata polisi uwanjani hapo katika kutekeleza majukumu
yao ni vema wakawa wakarimu licha ya kwamba wakati mwingine wamedaiwa
kutumia nguvu.
“Ni
vema sasa wakawa na ukarimu ndani yake ili mgeni adhibitiwe kistaarabu
kwa yule ambaye atakuwa ameshikiliwa kutokana na sababu yoyote akiwa
uwanjani hapo”.
Alisema
anatamani kuona kuanzia uwanja huo wa ndege hadi hotelini ambako mgeni
anakwenda anatumia muda mchache, anapata nafasi ya kuona picha za
viongozi mbalimbali ambazo zitakuwa uwanjani , picha za wanyama na video
zinaonesha utalii wa Tanzania.
“Kumpokea
mgeni jambo moja lakini namna ya kumhudumia ni jambo jingine na ndilo
muhimu zaidi.Tunataka mgeni afurahie kuwa Tanzania,”amesema.
Wakati
huo huo Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Nditiye alisema wizara
yao tayari imechukua hatua za kuondoa changamoto zilizopo ikiwamo ya
kufunga viyoyozi(AC) kwa ajili ya kuondoa hali ya joto.
Alisema
AC zilizopo ni za muda mrefu kwani ziliwekwa tangu majengo ya uwanja
huo yalipojengwa.Pia unafanyika ukarabati wa kuongeza eneo kwa ajili ya
wageni wanaosubiri kuhudumiwa.
Aliongeza
kuna jitihada ambazo Serikali inafanya za kuondoa msongamano wa wageni
ikiwamo ya kuharakisha ujenzi wa jengo jipya la kusafiria wageni la
Terminal III litakalohudumia watu milioni sita badala ya jengo la sasa
ambalo lengo lake lilikuwa kuhudumia watu milioni moja.
“Ujenzi
wa jengo jipya umekamilika kwa asilimia 70 na litakapokuwa tayari kwa
asilimia 100 litaanza kutumika kwani kasi ya ujenzi inakwenda
vizuri,’alisema.
0 comments:
Post a Comment