Mbunge
wa Jimbo la Mbozi (Chadema), mkoani Songwe, Pascal Haonga, amejitabiria
mabaya baada ya kuwataka wananchi kuchoma nyumba yake iwapo atahamia
Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Haonge
amewataka wananchi hao kufanya hivyo kutokana na baadhi ya viongozi wa
upinzani hususan madiwani na wabunge kujiuzulu na kuhama vyama vyao.
Idadi
kubwa ya madiwani wa upinzani wamejiuzulu na kuhama vyama vyao na
kujiunga na CCM wakati wabunge watatu hadi sasa wamejiuzulu na kuhama
vyama vyao ambao ni Godwin Mollel (Siha-Chadema) aliyehamia CCM, Lazaro
Nyalandu (Singida Kaskazini-CCM) aliyehamia Chadema na Maulid Mtulia
(Kinondoni-CUF) aliyejiuzulu na kujiunga na CCM.
Haonga
alitoa maelekezo hayo Jumamosi alipowahutubia wananchi wa Mji wa Mlowo
wilayani Mbozi, ambapo alisema hawezi kuwasaliti wananchi waliosimama
kidete kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa 2015 kuhakikisha anapata ushindi.
Alisema
wakati wa uchaguzi kulikuwa na matukio ya vurugu katika jimbo hilo huku
baadhi ya watu wakipoteza biashara zao, kujeruhiwa na wengine waliwekwa
ndani kwa ajili ya kupigania ushindi wake na wa Chadema, hivyo hawezi
kuwasailiti.
Aliwaponda
baadhi ya wabunge na madiwani wa chama hicho na vyama vingine vya
upinzani wanaohamia CCM kwa madai ya kuunga mkono Serikali ya awamu ya
tano kuwa hawatumii akili bali wanatumia matope.
“Najua
baada ya baadhi ya wasio na msimamo kuanza kuhamia CCM, mmepata hofu
kuwa hata kwangu itakuwa hivyo, niwahakikishie mimi siwezi kulamba
matapishi yangu, kuna watu mlipigwa mabomu ya machozi, kuna watu
walifungwa na kuna wengine walijeruhiwa kuhakikisha tunashinda, ikitokea
hivyo kateketezeni nyumba yangu,” alisema Haonga.
Aidha
Mbunge huyo alisema kuna baadhi ya viongozi wa CCM wanajinadi wanataka
kulirejesha jimbo hilo mikononi mwao na kwamba hawataweza kwa kuwa chama
hicho hakiaminiki tena na wananchi.
Alisema
kwa sasa wanajipanga kuhakikisha wanapata ushindi mkubwa kwenye
uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani, ili kujihakikishia ushindi zaidi
kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Aidha,
alisema anaendelea kuzitumia fedha za Mfuko wa Jimbo kuboresha
miundombinu zikiwamo zahanati, vyumba vya madarasa kwenye shule za
msingi na sekondari pamoja na barabara ili kuwapunguzia wananchi mzigo
wa kuchangia.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Mafunzo Chadema Kanda ya Nyasa, Mdude Nyagali, alisema
madiwani na wabunge wanaohamia CCM wakidai wanaunga mkono Serikali ya
awamu ya tano ‘wananunuliwa’.
Alisema
mbwembwe za viongozi wa CCM katika Mkoa huo kutaka kurejesha majimbo
yote ya upinzani kwenye uchaguzi Mkuu wa 2020 ni ndoto na haitatokea.
Vilevile
alisema baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM wanaodai Chadema
kinaelekea kufa, watakufa wao na sio chama hicho ambacho alidai
kinakubalika kila eneo kwa sasa tofauti na miaka iliyopita.
Alidai
uchaguzi wowote kura za CCM hazipo maeneo ya vijijini wala mjini bali
zipo kwenye vyombo vya Dola likiwemo Jeshi la Polisi.
“Watawezaje
kurejesha majimbo yetu wakati waliahidi milioni 50 kila kijiji,
zahanati kila kijiji na kuboresha miundombinu ya barabara ambayo mpaka
sasa hawajatekeleza?” Alihoji.
Diwani wa Kata ya Mlowo, Sebastian Kilindu, aliwataka wananchi wa kata hiyo kumkatakata mapanga endapo ‘atanunuliwa’ na CCM.
Alisema
kwa sasa ana misukosuko mingi ya kisiasa katika wilaya hiyo, hasa
kwenye vikao vya Baraza la Madiwani kwa madai baadhi ya viongozi wa
Halmashauri wanaongoza kimabavu.
0 comments:
Post a Comment