Askofu
Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe
amewaelezea waumini wake jinsi alivyohojiwa na timu mbili zilizoundwa
kwa nyakati tofauti na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Askofu
Kakobe, ambaye ameingia kwenye mgogoro na mamlaka za nchi tangu aeleze
kuwa ana utajiri mkubwa, alisema hayo wakati wa ibada iliyofanyika
katika kanisa lake lililopo Mwenge jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mara
ya pili kuzungumzia sakata hilo kwa waumini wake tangu Desemba 31 mwaka
jana.
Hata
hivyo, Kakobe alisema kutoa mrejesho huo hakuwazuii TRA kueleza
waliyobaini, lakini amesema ameona azungumze mapema na waumini wake kwa
kuwa ndio watoa sadaka na wana haki kwa asilimia 100 kujua
kinachoendelea kanisani kwao.
“Baada
ya kuleta barua, Januari 2, kiongozi wa tume iliyoundwa awali na kikosi
chake walifika na tuliwapa ushirikiano. Nilikuwa nao katika ofisi ya
kiuchungaji kwa mahojiano, walikuwa na karatasi za maswali na majibu
waliyaandika,” alisema.
“Waliuliza
kuhusu utajiri wangu, niliwaambia nina nyumba moja tu duniani ipo
Kijitonyama niliijenga kwa gharama ya Sh2 milioni na kiwanja nilinunua
Sh30,000. Ni nyumba ya kawaida na ipo katika mtaa wa kawaida uitwao kwa
Kakobe. Utafuteni mtaiona nyumba yangu.”
Askofu
Kakobe alisema aliwaeleza wazi kuwa ana waumini wake ambao
hawakuridhishwa na anapoishi, hivyo walitamani awe na sehemu nzuri
itakayoweza kufaa kwa ajili ya wageni wa kimataifa wanaoweza
kuwatembelea. Alisema walimshirikisha hilo na walijenga eneo jingine kwa
michango yao miaka 10 iliyopita.
Alisema
suala la akaunti za kanisa aliliweka wazi na kuwaambia kuwa kuna
akaunti benki ya NBC na akaunti ya mfuko wa kitaifa wa FGBF iliyopo pia
NBC Meru, Arusha.
“Niliwaambia
wazi mimi wala mke wangu hatuna akaunti benki. Binafsi sina mradi
wowote, sina shamba, sina kuku hata mmoja, paka na wala panya
niliyefuga. Niliwaambia hata kanisa hatuna mradi wowote wa kiuchumi na
hivi ndivyo tunavyoishi,” alisema.
“Mmoja
akaniuliza kwa nini hamna mradi wa kiuchumi, nilimweleza huo ni wito
wetu. Wakatoa karatasi moja ya kumbukumbu za TRA wakasema kuna shule
moja inaitwa Full Gospel si yenu? Nikasema hatuijui ila ni neno ambalo
linatumika kote duniani. Mkifuatilia vizuri mtajua wenye shule ni ya
kina nani.”
Alisema
walimuuliza iwapo ameajiri watu kanisani, akasema kuna watumishi zaidi
ya 1,000 ambao hawalipwi wanafanya kazi ya Mungu na huo ndiyo mfumo wa
kanisa.
Alisema
walimuuliza kuhusu ukusanyaji wa sadaka, maisha yake bila ya kuwa na
mradi wowote na baadaye waliitwa wakusanyaji sadaka kwa mahojiano zaidi.
“Wakauliza
kutoka kwa hicho kikosi ‘bahasha za maombi maalumu ambazo huelekezwa
kwa mchungaji zinakuwa nzito sana’, wakasema zinakuwa za kawaida tu.
Wakaniambia kwa uzoefu wako kiasi gani huwa kinapatikana kwa mwezi,
nikawaambia hufika hata Sh5 milioni lakini wakati mwingine kinaweza
kwenda chini.”
Alisema
baada ya hapo walihojiwa watoto na mke wake na kijana wake mmoja na
majibu yakawa yaleyale. Alisema walichukua baadhi ya kompyuta na nyaraka
muhimu kwa ajili ya uchunguzi na baadaye walitoa maoni yao.
“Kilichofuatia
ndicho kilichonifanya nitoe mrejesho kabla ya TRA. Yule kiongozi
niliyekabidhiwa na TRA alitoa ripoti inayoonyesha sina miradi wala
vyanzo vya fedha, kinachosalia ni sadaka na wao hawahusiki nazo,”
alisema Kakobe.
“Baada
ya kiongozi huyo kutoa ripoti hiyo, aliondolewa katika hiyo kazi na
hivi tunavyozungumza amepelekwa mkoani. Nikasema sasa nitamwaga mboga
leo, nikasema hapa kuna hila, nitaitungua ndege kabla haijapaa.”
Askofu
Kakobe alisema baada ya kiongozi huyo kutimuliwa ameletwa kiongozi
mwingine na kazi imeanza upya, “Wamekwenda nyumbani kwangu wamekagua
chumba kwa chumba, vyumba vyote nguo za wanangu, mke wangu; wanachambua
nguo mojamoja yaani wanasagula kama mtumbani. Wamekuja ofisini
hivyohivyo. Wameenda kwa viongozi wangu wamefanya hivyohivyo,” alisema.
Alisema wamehoji wapi anapeleka fedha na kuwapa mrejesho kuhusu safari zake za ndani na nje ya nchi lakini hawajaridhika.
“TRA
sasa ipo ndani ya sadaka. Hii ni TRA kweli? au kuna jambo? Mimi leo
nimemwaga mboga, hata (Askofu Josephat) Gwajima aliwahi kutoa mrejesho.
Sasa Gwajima na Kakobe ni mapacha. Walikuja ofisini wanakagua chumba
kimoja mara kingine nikasema watumishi tuwe macho wasijekutuwekea
bangi,” alisema.
Aidha
katika hatua nyingine, Askofu Kakobe aliwataka watumishi wa TRA kufuata
utaratibu na ikiwa wataanza kukusanya sadaka basi wakusanye makanisa
yote.
Alitoa onyo kwa watumishi hao na kusema wanamchonganisha Rais John Magufuli na wananchi wake kwa kuwa haamini kama wametumwa.
“Ninavyomjua
Rais John Magufuli ana hofu ya Mungu. Nalikumbuka neno lake la
‘mniombee nisiwe na kiburi’ na sijayasahau. Leo kama anatuma TRA
wachunguze sadaka sina imani hiyo. Tunajua kuna watu siku hizi
wanatafuta kiki, wanatafuta kupanda vyeo, nakushauri Rais wanaotafuta
vyeo kwa staili hii wageukie na uwatumbue,” alisema.
0 comments:
Post a Comment