Waziri
wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango jana tarehe 11 Januari,
2018 amewasilisha taarifa ya kamati aliyoiunda kuchunguza umiliki wa
kampuni ya simu Airtel kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. John Pombe Magufuli aliyeagiza kufanyika kwa uchunguzi huo tarehe
20 Desemba, 2017.
Baada ya kuwasilisha taarifa hiyo, Dkt. Mpango amesema Serikali imejiridhisha kuwa ubinafsishaji wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) kwenda Celtel, baadaye kuhamishiwa Zain na sasa Airtel ulifanyika kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu.
Kufuatia
ukiukwaji huo Dkt. Mpango amesema Serikali inayomiliki asilimia 40 ya
hisa za kampuni ya Airtel imeamua kufanya mazungumzo na kampuni ya
Airtel inayomiliki asilimia 60 ya hisa ili nchi iweze kupata haki yake.
“Lakini
niwaambie Watanzania yale ambayo tumeyaona ni machafu sana, ni mambo ya
hovyo kabisa, nchi yetu kwa kifupi tuliingizwa mkenge, ni fedha nyingi
zimepotea kwa hiyo sisi katika majadiliano haya lengo letu litakuwa ni
kuhakikisha Watanzania wanapata haki yao” amesema Dkt. Mpango.
Wakati huo huo,
Mhe. Rais Magufuli amepokea taarifa ya utekelezaji wa maagizo
aliyoyatoa tarehe 25 Novemba, 2017 wakati wa ufunguzi wa Hospitali ya
Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi
(Mloganzila) kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu.
Baadhi
ya maagizo hayo ni kupunguza baadhi ya idara na madaktari katika
hospitali ya Taifa Muhimbili na kuhamishia Mloganzila na hospitali za
mikoa kuhamishwa kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI) kwenda Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto.
Mhe.
Ummy Mwalimu amewasilisha taarifa hiyo akiwa ameongozana na viongozi
wakuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Mifupa (MOI), Taasisi
ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKHI), Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi
Shirikishi (MUHAS).
Katika hatua nyingine,
Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi amekamilisha kanuni
za sheria ya madini namba 7 ya mwaka 2017 na kuwasilisha vitabu vya
kanuni hizo kwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi.
Akiwa
na Naibu Mawaziri wa Madini Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo na Mhe. Doto
Mashaka Biteko, Prof. Kabudi amesema kanuni hizo zimekamilika siku moja
kabla ya tarehe ya mwisho iliyotolewa na Mhe. Rais Magufuli na
kubainisha kuwa sasa sheria inaweza kuanza kutumika.
Kwa
upande wao Naibu Mawaziri wa Madini wamewataka Watanzania na wadau wote
wa sekta ya madini kushirikiana na Serikali kutekeleza sheria hiyo na
wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kutoa msukumo wa kukamilishwa kwa
kanuni hizo.
0 comments:
Post a Comment