WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Majengo
Tanzania (TBA) Mhandisi Elius Mwakalinga akafanye tathmini ya ubora ya
jengo la kituo cha pamoja cha forodha cha Sirari kilichopo kwenye mpaka
wa Tanzania na Kenya.
Ametoa
agizo hilo jana (Jumapili, Januari 21, 2018) katika kikao cha
majumuisho ya ziara yake ya kikazi mkoani Mara, ambapo alimuagiza
Mkurugenzi huyo afanye tathmini na kuishauri Serikali kama jengo linafaa
kutumika.
Januari
17, 2018 Waziri Mkuu alikagua kituo hicho kilichopo wilayani Tarime
kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya, ambapo alisema hajaridhishwa na
ujenzi huo kwa kuwa upo chini ya kiwango.
Pia
Waziri Mkuu alipokagua jengo hilo alijionea mwenyewe kuta za jengo hilo
zikiwa na nyufa nyingi kuanzia ukutani hadi sakafuni na pia rangi za
baadhi ya kuta zikiwa zimebanduka. Kituo hicho kilianza kujengwa mwaka
2011 na kukamilika mwaka 2014
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu alizungumzia kuhusu miradi ya maji
inayotekelezwa katika mkoa huo, ambapo alisema “Miradi mingi ya maji
mkoani Mara ni ya hovyo na fedha nyingi zimetumika na wananchi
hawajapata huduma hiyo.”
Kufuatia
hali hiyo Waziri Mkuu aliwaelekeza viongozi wa mkoa huo ifikapo Januari
25, 2018 wamkabidhi taarifa ya mikakati waliyonayo ya kuondoa kero ya
maji kwa wananchi.
Pia
aliwaagiza Naibu Waziri, OR-TAMISEMI, Bw. Josephat Kandege na Katibu
Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Profesa Kitila Mkumbo wabaki mkoani
Mara ili wafuatilie miradi hiyo.
Alisema
anahitaji hatua sahihi zichukuliwe kwa waliohusika katika kukwamisha
miradi ya maji na watafutwe popote walipo akiwemo Mhandisi Emmanuel
Masanja aliyekuwa Halmashauri ya wilaya ya Rorya na kuhamishiwa
Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Waziri
Mkuu alisema mkoa huo una tatizo kubwa la maji hivyo ni vema vyanzo
vya maji vitunzwe ili visiharibiwe na shughuli za binadamu kama kilimo
na ufugaji.
Aliongeza
kuwa kutokana na usimamizi mbovu wa miradi ya maji, Serikali imevunja
Bodi ya Maji ya MUWASA na viongozi waliohusika katika usimamizi huo
pamoja na Wakandarasi husika wanahojiwa na vyombo vya dola.
0 comments:
Post a Comment