Naibu
Waziri wa Madini, Doto Biteko ametoa siku 14 kwa uongozi wa kiwanda cha
saruji cha Dangonte mkoa wa Mtwara kuingia mkataba na wachimbaji wadogo
wa gypsum.
Biteko ametoa kauli hiyo jana Januari 21, 2018 baada ya kutembelea kiwanda hicho na kuzungumza na viongozi wake.
Amesema
mikataba hiyo inapaswa kuwa na kipengele cha kuwalipa ndani ya siku 30
baada ya kiwanda kukusanya gypsum kutoka kwa wachimbaji hao, lengo
likiwa ni kuleta ufanisi na tija katika biashara zao.
“Nimekubaliana
hapa kamishna wa kanda atasimamia hili la mikataba kati ya kiwanda na
wachimbaji wa gypsum. Sehemu ya malipo itakuwa ndani ya mkataba na
watalipa ndani ya siku 30,” amesema.
Amesema wachimbaji hao wamekuwa wakilalamikia kucheleweshewa malipo yao baada ya kupeleka kiwandani bidhaa zao.
“Nimeambiwa
wachimbaji hawa walikuwa wanalipwa baada ya miezi mitatu lakini kwa
mkataba huu ambao wataingia na kiwanda sasa watakuwa wanalipwa ndani ya
siku 30,” amesema Biteko.
Amesema
Serikali ya Awamu ya Tano inalenga kuwasaidia wachimbaji wadogo
sambamba na wawekezaji ambao wanapaswa kufanya kazi bila kusumbuliwa.
“Uwepo
wa kiwanda hiki unawasaidia wachimbaji wetu waweze kupata bei nzuri
pamoja na kupata soko la uhakika la kuuza bidhaa zao. Dangonte
wameniahidi kwamba ndani ya muda mfupi watatekeleza agizo hili,”
amesema.
Biteko
amesema lengo la ziara yake ni kuwasaidia wachimbaji wa gypsum ambao
hawana mikataba na kujikuta wakibanwa katika uuzaji wa bidhaa zao.
0 comments:
Post a Comment