BARAZA
la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA- CCC) limesema
asilimia 90 ya malalamiko waliyoyapata, yanatokana na huduma za simu za
mkononi ikiwamo wananchi kutuma fedha bila jina kuonekana.
Katibu
Mtendaji wa TCRA-CCC, Mary Msuya, alisema hayo jana jijini Dar es
Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu malalamiko
waliyoyapata katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba mwaka jana.
Alisema
katika malalamiko hayo, watu wamekuwa wakilalamikia utumaji wa fedha
kwenda mitandao mingine bila jina kuonekana kabla ya kutuma jambo,
ambalo linawasababishia usumbufu pale wanapokuwa wamekosea kutuma fedha.
Alisema
jambo hilo tayari wameliwasilisha Benki Kuu (BoT) ili ichukue hatua kwa
wale ambao wanatuma fedha kupitia simu za mikononi kwa majina kuonekana
kabia ya kufanyika kwa miamala.
Alisema
mbali na suala hilo, pia kumekuwa na matangazo ya michezo ya
kubahatisha ambayo hutumwa kwenye simu kinyume cha utaratibu hali ambayo
inawakwaza watumiaji wa mawasiliano.
“Utakuta
mtu anasubiri ‘message’ (ujumbe) ya maana labda anategemea kupokea
muamala wa fedha. Matokeo yake inakuja ‘message’ ya ‘cheza biko’ au
‘tatu mzuka’. Kama mtu kacheza mara moja basi haina haja ya kuendelea
kumtumia ‘message’ kila mara au waweke ‘option’ (nafasi) ya mtu kujitoa
au waweke matangazo yao katika magazeti na si kuwasumbua watumiaji wa
simu za mikononi. Mbali na matangazo hayo ya kubahatisha yapo mengine
yanatumwa kinyume cha utaratibu,” alisema.
Aidha,
Msuya alisema kwa upande wa huduma za utangazaji, malalamiko yalihusu
kutokupatikana kwa chaneli za bure za kitaifa kupitia huduma ya digitali
mpaka mtumiaji alipie kinyume cha kanuni zinazotaka apate huduma hizo
bure bila gharama yoyote.
Alisema
licha ya serikali na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kuchukua hatua, bado
watumiaji wanapata changamoto ya kutakiwa kuongeza fedha ili kupata
king’amuzi kingine ili kuona chaneli za bure tofauti na ilivyokuwa
awali.
“Baraza
linapenda kutoa rai kwa watoa huduma kuhakikisha kuwa wanatoa taarifa
za kutosha kwa watumiaji ili kuwawezesha watumiaji kufanya maamuzi
sahihi na kupata huduma inayostahili.
"Watumiaji
wa ving’amuzi vya StarTimes wangepewa taarifa ya kutosha wakati wa
kununua ving’amuzi malalamiko yaliyopo sasa yasingekuwepo,” alisema Msuya.
Aidha,
Msuya alisema kampuni zinazotoa huduma za mawasiliano zinatakiwa kutoa
ushirikiano kwa baraza katika kushughulikia malalamiko ya watumiaji kwa
muda muafaka.
0 comments:
Post a Comment