Baraza
la Vyama vya Siasa limeunda kamati tano na kuzipa mwezi mmoja kupitia
mapendekezo ya Sheria mpya ya Vyama vya Siasa na Kanuni za usajili wa
vyama.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza
hilo, John Shibuda alisema kamati hizo zitafanya mapitio ya mapendekezo
ya sheria mpya na kanuni ndani ya wiki mbili ili kuona usahihi wa
vifungu vilivyopo.
Alisema baada ya mapitio hayo kamati hizo zinatakiwa zikamilishe maboresho ndani ya mwezi mmoja.
“Baraza
limezipa wiki mbili kamati ili ziweze kujipanga na kupitia mchakato
halafu ndani ya mwezi mmoja waweze kukamilisha na kutoa taarifa za
kutosha,” alisema Shibuda.
Alisema
baada ya maboresho kukamilishwa watatoa mapendekezo kwa mwenyekiti
ambaye ataitisha kikao na kuyajadili kisha itaandaliwa rasimu.
Shibuda
alisema, hadi sasa mchakato wa kutunga sheria na kanuni za usajili wa
vyama vya siasa bado haujatekelezwa na badala yake zimeunda kamati
ambazo zitachakata mapendekezo.
“Hadi
sasa tunaendelea na sheria na kanuni zilezile za usajili wa vyama vya
siasa, mapendekezo yaliyokuja kutoka sekretarieti yanaenda kuchakatwa na
kamati ya sheria na Utawala Bora ya baraza,” alisema Shibuda.
Alisema baraza ndilo litakaloridhia yapi yanafaa kuwa mapendekezo ya vyama vya siasa kwa ajili ya kutungwa kwa sheria.
Shibuda
alisema baraza hilo lipo huru na vyama vyote vimeshiriki wakiwamo
wajumbe kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao wamewakilishwa
na Salum Mwalimu ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar (Chadema) na
wajumbe wengine kutoka vyama mbalimbali.
Amezitaja
kamati zilizoteuliwa na viongozi wake ni Kamati ya Bunge na Siasa,
Mwenyekiti Juju Martini Danda (NCCR-Mageuzi) na Makamu Mwenyekiti ni
Mohamed Masoud Rashid (Chauma).
Nyingine ni kamati ya Sheria na Utawala Bora ambapo mwenyekiti wake ni Hassan Almas (NRA) na Makamu wake ni Said Sudi.
Shibuda
aliitaja pia Kamati ya Maadili na Mahusiano inayoongozwa na Mohamed
Ally Abdallah (Demokrasia Makini) na Peter Magwira (Democratic Party).
Kamati
ya fedha Mwenyekiti John Cheyo (UDP) na Salum Mwalimu ambapo ile ya
Uongozi wa Baraza la vyama vya Siasa, Shibuda na Dk. Abdallah Juma
Saadala.
Katibu
Mkuu wa Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC), Doyo Hassan
alisema hajaona sababu za mapendekezo hayo kuundiwa kamati.
0 comments:
Post a Comment