Mvua zinazoendelea kunyesha nchini zimesababisha madhara katika Mikoa ya Arusha na Manyara.
Katika
Mkoa wa Arusha, mvua hizo jana zilisababisha shughuli za maendeleo
katika Barabara Kuu ya Arusha kwenda Karatu, kusimama kwa muda, baada ya
kingo za daraja linalounganisha Mji wa Mto wa Mbu na Makuyuni kusombwa
na mafuriko.
Kutokana
na hali hiyo, abiria wanaotoka na kwenda mkoani Mara, watalii
wanaotembelea Hifadhi za Manyara, Serengeti, Ngorongoro pamoja na
wananchi mbalimbali, walijikuta katika wakati mgumu wa kuendelea na
shughuli zao za kila siku kutokana na ubovu wa barabara hiyo.
Kukatika
kwa daraja hilo ambalo ni kiungo muhimu cha shughuli za maendeleo,
kulisababishwa na mvua kubwa iliyonyesha maeneo ya milimani, wilayani
Monduli na kusababisha magari zaidi ya 300 kushindwa kupita kwa wakati.
Akizungumzia
athari hizo kwa njia simu, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania
(TANROADS), Mkoa wa Arusha, Mgeni Mwanga alisema baada ya uharibufu wa
barabara hiyo, wamefanikiwa kuweka kifusi katika eneo hilo na magari
yalianza kupita, kuanzia jana saa sita mchana.
“Usiulize ukiwa mbali, njoo hapa ‘site’ uone kwa macho yako kama kweli kuna daraja limesombwa na mafuriko kama unavyouliza.
“Kimsingi, daraja halikukatika ila kingo zake ndizo zimemegwa na maji baada ya maji kujaa kupita kiasi.
“Yaani,
hivi ninavyozungumza na wewe, tunamalizia kujaza kifusi na magari yote
yalishaanza kupita na kuendelea na safari,” alisema Mwanga.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Isack
Joseph, alisema kukatika kwa daraja hilo kulisababisha madhara kwa
wananchi wilayani kwake.
“Maeneo
mengi wilayani Monduli yalikuwa na mvua kubwa sana jana usiku na kwa
kuwa wilaya ina maeneo yenye milima, maji yaliteremka kwa wingi kuelekea
chini.
“Kazi
ya kutafuta njia mbadala ili kuruhusu magari na watumia barabara
waendelee na shughuli zao, zinafanywa kwa ushirikiano wa TANROADS na
halmashauri,” alisema Joseph.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Iddi Kimanta alisema jitihada za kurudisha
usafiri katika hali ya kawaida zilifanikiwa na magari kuanza kupita.
Pamoja
na hayo, Kimanta alisema Serikali ya Wilaya ya Monduli inaendelea
kufuatilia madhara ya mvua hizo na itatoa msaada kwa waathirika pindi
utakapohitajika.
0 comments:
Post a Comment