Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu kifungo cha miaka mitano jela au
kulipa faini ya Sh6 milioni, wafanyabiashara wawili, Naushad Mohammed
Suleiman (63) na Ali Makame Juma (36) baada ya kupatikana na hatia ya
kusafirisha vipande saba vya madini ya dhahabu vyenye thamani ya Sh
989.7 milioni bila kuwa na leseni.
Pia,
mahakama hiyo imetaifisha dhahabu yote iliyokamatwa pamoja na mabegi
mawili ya fedha mbalimbali kutoka nchi 15 duniani, walizokamatwa nazo,
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aman Karume uliopo Zanzibar.
Hukumu
hiyo imetolewa jana Alhamisi, Januari 11 na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard
Mashauri baada ya washtakiwa hao kukiri mashtaka yanayowakabili.
“Ili
iwe fundisho kwa watu wengine, katika kosa la kwanza mahakama
inawahukumu kulipa faini ya Sh.milioni 2 ama jela miaka 2, pia kosa la
pili faini Sh.mil 4 ama jela miaka 3, mkishindwa mtaenda jela na
kutumikia vifungo hivyo sambamba,” Alisema Hakimu Mashauri
Wafanyabiashara
hao maarufu ambao ni wakazi wa Zanzibar, walikuwa wanakabiliwa na
makosa mawili, ambayo ni kula njama na kusafirisha madini nje ya nchi
kinyume cha sheria na bila kuwa na leseni kutoka mamlaka husika.
Washtakiwa
wanadaiwa kukamatwa Novemba 29, 2017, katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Aman Karume, wakisafirisha madini hayo kwenda Dubai katika
Falme za Kiarabu.
Hata hivyo, wafanyabiashara hao walilipa faini na kuepuka kifungo hicho.
0 comments:
Post a Comment