ACT
Wazalendo kimetofautiana na (CHADEMA) kuhusu kushiriki katika uchaguzi
wa marudio ambao unatarajiwa kufanyika Februari 17, 2018 katika jimbo
la Kinondoni na Siha. ACT Wazalendo wanasema kushiriki uchaguzi huo ni
kuhalalisha mchakato haramu
Akizungumza
na waandishi wa habari leo, Naibu Katibu Mkuu (Bara) ACT Wazalendo
ndugu Msafiri Mtemelwa amesema kuwa uwanja wa Demokrasia nchini bado si
sawa na kuwa kushiriki uchaguzi huo ni kuhalalisha mchakato haramu,
hivyo wao ACT Wazalendo hawapo tayari kuhalalisha jambo.
"Chama
cha ACT Wazalendo kimeona ni jambo muafaka kutoa ufafanuzi kwa
wanachama wake na wananchi kwa ujumla kuhusu nafasi na msimamo wake
kwenye uchaguzi wa marudio kwenye Majimbo ya Kinondoni na Siha na Kata
tisa uliopangwa kufanyika tarehe 17 Februari, 2018. Ikumbukwe kuwa
Kamati ya Uongozi ya ACT Wazalendo iliyoketi tarehe 8 Novemba 2017
iliamua kusitisha ushiriki wa Chama chetu kwenye uchaguzi wa tarehe 13
Januari 2018 na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu kufanya tathmini
na uamuzi juu ya Chama kushiriki kwenye chaguzi za marudio. Ni Jambo la
kiukombozi kwamba baadhi ya vyama vya upinzani navyo vilichukua mkondo
huo wa kugomea uchaguzi"
Mtemelwa
aliendelea kusisitia kuwa wao waliamua kujitoa kwenye uchaguzi huo
kutokana na vyombo vya dola kuingilia mchakato wa uchaguzi na
kulazimisha ushindi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
"Hata
hivyo tunatambua kuwa kutoshiriki chaguzi tu haitoshi kwani haijibu
swali la nini kinafuata baada ya kususia. Chama chetu pia kinatambua
kuwa Chama tawala kinaweza kufurahia kususiwa na kuna uwezekano mkubwa
wa kuendelea kubinya demokrasia ili vyama vya upinzani viendelee kususia
chaguzi zinazokuja. Kamati Kuu imeuagiza Uongozi wa Taifa wa Chama
kuwafikia wadau wote wa demokrasia nchini na kuweka mikakati ya pamoja
ya hatua za ziada za kuchukua ili kuboresha mazingira ya chaguzi za haki
nchini kwetu pamoja na kuweka shinikizo kubwa kwa serikali kufanya
mabadiliko muhimu ya kisheria, kiutendaji na kikatiba ili kuweka sawa
uwanja wa mapambano ya kidemokrasia"
Kutokana na mambo hayo ACT Wazalendo wakaweka msimamo wao
"Hivyobasi,
tunapenda kuweka bayana kwamba Chama chetu hakitoshiriki kwenye
uchaguzi wa marudio wa tarehe 17 Februari kwenye Majimbo ya Kinondoni,
Siha na udiwani kwenye Kata tisa. Msimamo huu unatokana na ukweli kwamba
sababu zilizolalamikiwa kwenye uchaguzi wa 13 Januari, 2018
hazijabadilika kwa sehemu kubwa. Mageuzi madogo yaliyofanywa na Tume ni
kauli yao kuwataka Wakuu wa Wilaya kuacha kuingilia uchaguzi. Hili ni
tone dogo katika malalamiko ya vyama vya upinzani dhidi ya Tume" alisema Mtemelwa
Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo chenyewe kimetangaza kushiriki uchaguzi huo
wa marudio katika majimbo mawili Kinondoni na Siha na tayari
wameshachukua fomu Tume ya Uchaguzi na kuzirudisha.
0 comments:
Post a Comment