WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewakemea watumishi wa umma na madiwani ambao
wameunda makundi ndani ya Manispaa ya Songea kwa kuweka mbele maslahi
yao binafsi na akawataka wajirekebishe mara moja.
Ametoa onyo hilo jana (Jumamosi, Desemba 23, 2017) wakati akizungumza na
watumishi wa manispaa na madiwani kwenye kikao kilichofanyika kwenye
ukumbi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Songea, mjini Songea mkoani
Ruvuma.
“Watumishi wa umma ni lazima muelewe kwamba katika Halmashaurti zenu
mnafanya kazi na waheshimiwa madiwani sababu mnatekeleza Ilani ya Chama
cha Mapinduzi, na mnapotekeleza majukumu yenu mzingatie maslahi ya umma.
Mnalo jukumu la kuhakikisha Halmashauri yenu inaongozwa kitaalamu,”
alisema.
“Nanyi waheshimiwa madiwani, mtambue kuwa mnaongoza wataalamu wa fani
tofauti. Lakini hapa Songea, madiwani mmeigawa Halmashauri, mnaiendesha
vibaya. Miradi haiendi vizuri kwa sababu mmejiingiza kwenye kujali
maslahi yenu binafsi,” alisema Waziri Mkuu.
“Mmebishana sana katika miradi ya maji, ujenzi wa kituo cha mabasi kwa
sababu kila mmoja anataka mtu wake aingie. Wakati mwingine pesa
zinatumwa, nyie mnaanza kubishana tu, sasa ni mwisho. Mkitaka
kutuangusha Serikali, ama tutawafukuza uanachama ama tutavunja
Halmashauri. Tunao uwezo wa kulivunja Baraza la Madiwani,” alionya.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo,
Bi. Tina Sekambo kwa uamuzi wake wa kuruhusu mradi mmoja uendelee baada
ya kuona kuna malumbano ya kimaslahi miongoni mwa madiwani.
“Mkurugenzi chapa kazi, na usimuogope mtu yoyote, iwe ni Diwani au
Mstahiki Meya. Simamia sheria kama ulivyofanya kwenye mradi ambao
ulileta maneno, ukaamua Naibu Meya asaini nyaraka, na mradi ukaendelea.
Kisheria, Naibu Meya anaruhusiwa kusaini,” alisema.
Waziri Mkuu alisema kuwa Serikali inakusanya kodi ili wananchi wapate
maendeleo na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haina subira na mtu
anayeharibu kazi. Aliwaagiza Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa
wasimamie kazi na yeyote atakayeleta uzembe, wamripoti kwake.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuonya Afisa Elimu wa Manispaa
hiyo, Bi. Edith Kangomba na kumtaka aache tabia ya kuchochea migomo kwa
madiwani.
“Mkurugenzi wa Manispaa mpe taarifa akirudi kwamba tutamfukuza kazi kwa
sababu anashirikiana na baadhi ya madiwani kuleta migomo kwenye
utekelezaji wa miradi. Mwambie leo ninamuomya, siku nyingine nitamfukuza
hapa hapa kwenye kikao,” alielekeza Waziri Mkuu kwa vile Afisa Elimu
huyo hakuwepo kwenye kikao hicho kwa sababu yuko likizo.
“Nasema hivi kwa sababu hao washirika wake, wako hapa hapa na wamesikia
ujumbe huu. Serikali inahangaika, tunaleta fedha ajili ya elimu, lakini
zikifika mnachaguana, na Manispaa yenu iko nyuma kielimu,” alisema.
Aliwataka wakuu wa idara wasimamie idara zao na kuziongoza kwa uadilifu
na kuwaeleza kuwa Serikali inatambua upungufu wa watumishi unaozikabili
Halmashauri nyingi uliosababishwa na zoezi la uhakiki wa vyeti.
“Tunaajiri kidogo kidogo kwa awamu ili kuziba pengo la vyeti feki.
Tunajua sekta za afya na elimu ndizo zimeathirika zaidi. Lakini
nasisitiza tena, tunataka watumishi waadilifu, waaminifu na
wawajibikaji. Endeleeni kuchapa kazi,” alisisitiza.
Waziri Mkuu alimaliza ziara yake ya siku moja mkoani Ruvuma jana hiyohiyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, DESEMBA 24, 2017
0 comments:
Post a Comment