Kampeni
za ubunge na udiwani zikiendelea, mgombea udiwani (Chadema) Kata ya
Buhangaza wilayani Muleba amepotea katika mazingira ya kutatanisha.
Imeelezwa alipotea Februari 2,2018 alipokuwa akitokea Bukoba mjini kwenda nyumbani kwake Kijiji cha Buhangaza ikidaiwa ametekwa.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Isack Msangi amethibitisha kupokea taarifa za kupotea kwa mgombea huyo.
Amesema kuwa hawana madai kuwa ametekwa bali aliondoka nyumbani na hajarejea.
Msangi
amesema polisi inawaomba wananchi kutoa ushirikiano bila kupotosha au
kuegemea upande mmoja wa kisiasa kwa kutuhumu upande mwingine bali
waungane kufanikisha kupatikana kwake.
Katibu
wa uenezi wa Chadema jimbo la Muleba Kusini na mratibu wa chama hicho
jimbo la Muleba Kaskazini, Hamisi Yusufu amesema leo Februari 4,2018
kuwa mgombea huyo ni Athanasio Makoti (28).
Yusufu
amesema Makoti ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la AGT anashiriki uchaguzi
mdogo wa udiwani utakaofanyika Februari 17. Anachuana na mgombea wa
CCM, Jenitha Tibeyenda na wa NCCR -Mageuzi, Grason Anaseti.
Amesema
Februari 2,2018 saa 12:00 jioni akitumia simu yake ya mkononi
aliwajulisha viongozi wa Chadema ngazi ya wilaya kuwa alipanda gari
lenye watu wanne kutoka Kijiji cha Mafumbo njia panda ya kwenda
Kamachumu akielekea Kijiji cha Buhangaza.
Yusufu
amesema baadaye ujumbe mfupi wa maneno (sms) ulitumwa kwa Advera
Kalikwela, diwani wa viti maalumu (Chadema) Kata ya Ijumbi ukieleza,
“Nimeteremka hapa Mafumbo kabla ya kufuatwa na bodaboda wangu
nimezingirwa na gari lenye watu wanne mmoja mwanamke, mbele dereva wa
kiume na vijana wengine wawili ni kama nimetekwa.”
Amesema
baada ya ujumbe huo, simu ya Makoti iliita bila kupokewa na hadi sasa
hakuna taarifa za kuonekana kwake na kwamba familia ilitoa taarifa
polisi.
Egbert
Makoti ambaye ni mdogo wa mgombea huyo amesema baada ya kuchukua fomu,
ndugu yake aliwaeleza kuna watu ambao hakuwataja waliomtaka aachane na
kata hiyo wakimtaka apokee Sh8 milioni lakini alikataa.
Katibu
wa Baraza la Wazee la Chadema, Rodrick Lutembeka amesema chama hicho
kitaendelea kumnadi katika kampeni zinazoendelea katika Kata ya
Buhangaza.
Kata
hiyo ina vijiji vitatu vya Buhangaza, Kashenge na Buyaga ikiwa na
vitongoji 13 ikikadiriwa kuwa na zaidi ya wapiga kura waliojiandikisha
2,500.
Credits: Gazeti la Mwananchi
0 comments:
Post a Comment