Askofu
wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini
Mashariki, Lucas Mbedule amewaomba msamaha washarika wa Kanisa Kuu la
Mtwara ili wasiliumize kanisa.
Amewataka kumaliza tofauti zao na kukutana katika ibada wakiwa na mioyo minyenyekevu kumwomba Mungu.
Baadhi ya waumini wa kanisa hilo wamekuwa na mgogoro wakimpinga askofu huyo kwa takriban miaka miwili.
Waumini hao wamemwomba Askofu Mkuu wa KKKT, Fredrick Shoo kwenda kuzungumza nao na kuunda tume ya uchunguzi.
Agosti
28,2016 baadhi ya waumini na wazee wa kanisa waliingia katika ibada
wakiwa na mabango yaliyokuwa na ujumbe wa kumpinga askofu huyo kwa
tuhuma za kukiuka katiba, unyanyasaji wa watumishi na ubadhirifu wa
fedha za usharika na dayosisi.
Umoja wa wazee ulitoa tamko kumwomba mkuu wa kanisa kufanya uchunguzi.
Akizungumza
wakati wa ibada leo Februari 4,2018, Dk Mbedule amewaomba wote
aliowakosea wamsamehe, awali akiingia kanisani alilala kifudifudi
mlangoni na kusali.
Amesema
watakapoweka vizuri utaratibu, Dk Shoo atakwenda kuwasalimia na
kuzungumza nao kwa kuwa mazungumzo yanaruhusiwa lakini yasiharibu
utaratibu wa ibada.
“Nimewakosea
mengi siwezi kuhesabu kabisa, mimi ni mwenye dhambi kabisa kabisa
sistahili kabisa. Naomba mnisamehe tusilitese kanisa, kuna jambo njoo
uniambie hakuna ambaye nimemkataza awe mzee wa kanisa, mchungaji au
yeyote hakuna ambaye nimemfungia mlango,” amesema Dk Mbedule.
Amesema,
“Moyo wangu uko tofauti na sura yangu, naomba nirudie tena tofauti
ndogo za sisi za kibinadamu, sisi si malaika zisitufanye tulitese kanisa
wala kuliingiza katika gharama kubwa, ukiniambia nimekosa nitasema na
kama ni kujieleza nitajieleza, narudia tena wale wote waliojikwaa na
mimi kwa kuwatazama au kwa kusema naomba unisamehe tutazame mbele, mimi
sijaumbwa kama malaika nimeumbwa kama binadamu wengine yeyote anayekosa
kwa kusema, anayekosa kwa kuwaza au kutenda.. mimi si mtakatifu hizi
gwanda (akionyesha mavazi ya kiaskofu aliyovaa) mmenipa ninyi kwa njia
ya vyombo vya dayosisi.”
Kabla
ya kuomba msamaha jana, baadhi ya waumini wa kanisa hilo walionekana
kwenda kinyume cha mwongozo wa ibada na hata kujikuta wakipishana katika
kuimba.
Awali,
akihubiri Mkuu wa Jimbo la KKKT Pwani, Mchungaji Zacharia Lyakunge
alisisitiza kudumisha amani kwa kanisa na Taifa kwa jumla.
“Amani
ni kitu cha thamani mno, amani ni uzima wetu, amani ni baraka zetu,
kwenye ndoa zetu kama hakuna amani hakuna furaha ya ndoa; kwenye kazi
zetu kama hakuna amani hatutaiona furaha ya kazi; kwenye taasisi, jamii
kama hakuna amani hakuna chochote tutakachokifanya. Tukitaka baraka na
mafanikio katika maisha yetu tumng’ang’anie huyu Yesu, ukiishi na Yesu
hutahesabu mabaya, hutakumbuka mabaya, ukiishi na Yesu utakumbuka zuri
alilolileta duniani,” amesema Mchungaji Lyakunge.
Na Haka Kimaro, Mwananchi
0 comments:
Post a Comment