Umoja
wa Afrika (AU) umelaani matamshi ya dharau na kuishushia hadhi Afrika
aliyotoa Rais Donald Trump alipokutana na wabunge kwenye ofisi yake ya
mviringo ikulu.
Vyombo
vya habari vya Marekani yakiwemo mashirika makubwa kama CNN na
Washington Post yalinukuu vyanzo vya uhakika kwamba Trump aliyaita
mataifa ya Haiti, El Salvador na Afrika kuwa “mataifa machafu”.
Katika
kikao hicho Alhamisi iliyopita Trump inadaiwa alihoji: “Kwa nini
tunawaruhusu watu hawa kutoka “nchi chafu” kuingia nchini?”
Botswana
imekuwa nchi ya kwanza Afrika kumshutumu Trump kwa kuyaita mataifa ya
Afrika kuwa "machafu" na ikasema tamko la rais huyo ni la kukosa
kuwajibika, linakera na uthibitisho wa "ubaguzi wa rangi".
Pia
imechukua hatua ya kumwita balozi wa Marekani aliyeko Botswana aweze
kufafanua iwapo Marekani inachukulia taifa hilo la kusini mwa Afrika
kama "taifa chafu" na taifa la mabwege.
Botswana imeitaka jumuiya ya kiuchumi ya nchi za kusini mwa Afrika Sadc pamoja na Umoja wa Afrika kushutumu tamko hilo la Trump.
Taarifa ya AU
Umoja
wa Afrika, katika taarifa yake Ijumaa ilisema Afrika inasikitishwa na
matamshi ya Rais wa Marekani na imemtaka “afute matamshi” hayo na
“awaombe radhi Waafrika.”
“Umoja
wa Afrika unalaani vikali matamshi yasiyo ya heshima na inamtaka
ayafute na pia awaombe radhi siyo tu Waafrika, bali watu wote wenye
asili ya Afrika walioko duniani kote,” ilisema taarifa hiyo.
Ebba
Kalondo, ambaye ni msemaji wa mwenyekiti wa AU Moussa Faki, mapema
aliliambia shirika la AFP kwamba kauli ya Trump “haikubaliki”.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Rupert Colville amesema tamko hilo la Trump ni la kushangaza, la aibu na la ubaguzi wa rangi.
Colville
amesema: "Iwapo yatathibitishwa, matamshi haya ni ya kushangaza na ya
aibu sana kutoka kwa Rais wa Marekani; nasikitika kwamba hakuna maneno
mengine ya kueleza hili ila kusema kwamba ni ubaguzi wa rangi.”
Colville
alizungumzia hotuba ya Trump wakati wa kampeni 2016 ambapo alisema
wahamiaji kutoka Mexico ni wahalifu na wabakaji. Trump alitoa matamshi
hayo alipokutana na wabunge kutoka vyama vyote kujadili pendekezo la
mpango wa wahamaiji usiopendelea upande wowote.
Baadaye
Trump kupitia Twitter yake alijitetea kwa kusema hakutumia maneno hayo,
lakini akasema aliyoyasema alitumia "lugha kali".
0 comments:
Post a Comment