Spika Job Ndugai leo amelazimika kumpokonya Najma Giga uongozi wa kikao cha Bunge baada ya mzozo uliosababishwa na mbunge wa CCM aliyewafananisha wapinzani na mbwa.
Spika Ndugai alifanya kitendo hicho kisicho cha kawaida katika kikao cha 44 cha Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge wakati wa kujadili hotuba ya bajeti ya mwaka 2018/19 ya Wizara ya Fedha na Mipango.
Wakati akichangia, mbunge huyo wa Jang’ombe, Ali Omar alisema: “Ukiona majuha wanapongezana wakaona wamefanya la maana, kuna hawa mbwa kama tutawatoa itakuwa vizuri sana. Nasikia milio ya mbwa ukiwatoa itakuwa vizuri.”
Baada ya kauli hiyo, wabunge wawili kutoka Chadema, Joseph Selasini (Rombo) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) walisimama kutaka utaratibu ufuatwe kwa mchangiaji kuomba radhi.
Hata hivyo, Giga hakuruhusu hilo na kusababisha wabunge wengine wa upinzani kupiga kelele wakimtaka mbunge huyo afute kauli hiyo.
Giga alitumia kama dakika mbili kuwazuia lakini hakuweza na kumtaka Omar aendelee kuchangia.
Hata hivyo hakuweza kuwazuia kutokana na wabunge hao wa upinzani kuendelea kupiga kelele wakisisitiza Omar ashinikizwe kufuta kauli yake.
Wakati kelele zikiendelea na utulivu bungeni ukitoweka, Spika Ndugai akaingia na kuchukua uongozi wa kikao na hivyo Giga, aliyeanza kuongoza kikao hicho tangu asubuhi, kulazimika kumuachia uongozi.
Credit: Mwananchi
Advertisement
0 comments:
Post a Comment