Serikali
ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na Kampuni ya Total wamekubaliana
kuharakisha hatua zote za awali katika Mradi wa Bomba la Mafuta kutoka
Uganda hadi Hoima Tanga ili shughuli za ujenzi rasmi zianze mwezi Mei
mwaka huu.
Makubaliano
hayo yalifikiwa Alhamisi, Februari 1, wakati Waziri wa Nishati, Dkt.
Medard Kalemani alipokutana na uongozi wa juu wa kampuni hiyo wizarani
Dodoma.
Aidha,
makubaliano mengine yaliyofikiwa katika kikao hicho ni kuwa kazi za
awali za maandalizi ya ujenzi ziwe zimekamilika ifikapo mwezi Machi
mwaka huu.
“Ni
lazima tuharakishe mchakato huu kama Mheshimiwa Rais Magufuli
alivyoagiza. Hivyo, tumekubaliana kwamba shughuli zote za maandalizi
ziwe zimekamilika ifikapo Machi mwaka huu ili kuwezesha shughuli rasmi
za ujenzi wa Bomba kuanza mwezi Mei,” alifafanua Waziri Kalemani.
Vilevile,
katika kikao hicho, Rais wa Kampuni ya Total sehemu ya Afrika, Guy
Maurice ambaye alikuwa kiongozi wa Ujumbe huo, alibainisha nia ya
kampuni yake kuwekeza katika shughuli nyingine mbalimbali zinazohusiana
na Mradi wa Bomba jambo ambalo alisema litainufaisha zaidi Tanzania.
Mbali
na makubaliano yote yaliyofikiwa, Waziri Kalemani pia alisisitiza kuwa
ni muhimu kampuni ya Total iwasilishe Mpango-Kazi wake wizarani mapema
iwezekanavyo ili utumike kama mwongozo-rejea katika kutathmini
utekelezaji wa Mradi huo mkubwa.
Kampuni ya Total ndiyo mwekezaji katika utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Uganda hadi Hoima, Tanga.
Kikao
hicho pia kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt.
Hamisi Mwinyimvua, Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Wizara Lusius
Mwenda, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Haji Janabi na maafisa wengine
waandamizi kutoka wizarani.
0 comments:
Post a Comment