Serikali
imetoa pole kwa familia ya mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha
Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline aliyeuawa kwa kupigwa risasi
Februari 16,2018 na kuahidi kugharimia mazishi yake.
Akizungumza
leo Februari 18,2018 na vyombo vya habari, Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema pamoja na katibu mkuu wa
wizara watahakikisha wanasimamia shughuli zote za msiba huo.
Amesema Akwilina alikuwa katika majukumu yake ya kawaida akipeleka barua yake ya mafunzo kwa vitendo Bagamoyo alipofariki dunia.
"Mafunzo
yake kwa vitendo yalikuwa yanatarajiwa kuanza Februari 26, mwaka huu,
hivyo kifo chake kimeleta simanzi kwa wananchi wote na Serikali kwa
jumla.”
"Akwilina
alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wa kike waliojipambanua kwa kujua
umuhimu wa elimu, alihakikisha anasoma kwa bidii kwa manufaa yake na
familia yake, lakini pia alinufaika na mkopo wa elimu ya juu," amesema
Profesa Ndalichako.
Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema uchunguzi wa
tukio hilo utafanyika haraka iwekezanavyo, kwa weledi na utaalamu ili
haki itendeke.
"Tutafanya
uchunguzi na kuwachukulia hatua kali za kisheria wote watakaobainika
kuhusika na tukio hilo, Serikali tunasikitishwa na kifo cha mwanafunzi
huyu, pia na kujeruhiwa raia na askari polisi wawili," amesema Masauni.
Amesema Serikali haiwezi kuyaacha matukio hayo yapite kama yalivyo, hivyo imeyachukulia kwa uzito unaostahili.
0 comments:
Post a Comment