Balozi mteule, Dk Willibrod Slaa amesema amekuja nchini kwa ajili ya kushughulikia usajili wa Hospitali ya CCBRT.
Katibu
mkuu huyo wa zamani wa Chadema, ametoa kauli hiyo leo Februari 6, 2018
wakati akihojiwa katika kipindi cha 360 kinachorushwa na Kituo cha
Televisheni ya Clouds.
“Familia
yangu nimeiacha Canada, wengine wanajua, sikuja kwa sababu ya ubalozi.
Mimi ni mwenyekiti wa CCBRT ndicho kimenileta na wengine mnafahamu
katika nchi yetu mengi yanafanyika,” amesema.
Novemba
23 mwaka jana, Rais John Magufuli alimteua Dk Slaa kuwa balozi, lakini
mpaka sasa hajaapishwa na kupangiwa kituo cha kazi.
Dk
Slaa ambaye kwa sasa anaishi Canada alitangaza kuachana na siasa
kutokana na kutofautiana na chama chake katika kumpokea Edward Lowassa
aliyehama kutoka CCM na baadaye kupitishwa kuwa mgombea urais kupitia
muungano wa Ukawa.
Alisema chama chake hakikutekeleza makubaliano waliyoafikiana ya kuwapokea baadhi ya makada wa CCM akiwamo Lowassa.
Januari
29, 2018, Dk Slaa alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli,
Ikulu Dar es Salaam na kumshukuru kwa kumteua kuwa Balozi na kuahidi
kuwa yupo tayari kutekeleza majukumu atakayopangiwa kwa kutanguliza
maslahi ya Taifa.
Katika
kipindi hicho, Dk Slaa ameulizwa kama amekuja kula kiapo na kupangiwa
kituo cha kazi, lakini amepinga jambo hilo na kubainisha kuwa amekuja
kushughulikia usajili wa hospitali hiyo kwa kuwa yeye ni mwenyekiti wa
bodi.
Amesema kwa mujibu wa mabadiliko ya sheria, CCBRT inatakiwa kujiandikisha upya vinginevyo itafutwa.
Kuhusu
taarifa kuwa ameajiriwa katika duka kubwa la bidhaa za nyumbani
(Supermarket) la Costco lililopo Oakville, Toronto nchini Canada,
amesema: “Hizo ni propanganda nisingependa kuzizungumza lakini
Supermarket inayozungumzwa si kama mnavyofikiri ni kubwa.
“Kitu
kikubwa tunatofautiana katika mtazamo, fikra tunavyofanya vitu vyetu.
Canada haina mwenyewe kuna raia wa kutoka kila nchi. Sisi hapa tunasema
hapa kazi tu lakini kule ni maisha. Unakuta waziri anatoka ofisini kwake
anakwenda kufanya kazi nyingine, baadaye anatoka na kwenda kufanya
nyingine. Kufanya kazi tatu ni kawaida.”
Ametolea
mfano ufanyaji kazi wa Canada na Tanzania amesema baadhi ya Watanzania
huingia ofisini na kusoma magazeti, au kutumia simu kufanya biashara
zao.
“Canada
utaingia ofisini na simu au ipad lakini utaiacha getini na matokeo yake
nchi ile ni matajiri. Watu ni matajiri kila mtu ana utambuliso wa
maisha mazuri ni kwa sababu wanafanya kazi na huduma zote ziko vizuri,”
amesema.
Kuhusu
kufunga ndoa amesema: “Siasa za Tanzania zilichangia mimi kutokufunga
ndoa kwa kipindi chote lakini Februari 2016 kule Canada nilifunga ndoa
(na Josephine Mushumbusi), ile si ndoa kwani tulishakaa, kanisa
ilichokuja kufanya ni kuhalalisha tu.”
0 comments:
Post a Comment