Asiilimia
2.7 ya wafungwa na mahabusu waliopimwa virusi vya Ukimwi (VVU) kwa
mwaka 2016/17 wamegundulika kuwa na virusi vya ugonjwa huo.
Matokeo
hayo yamebainika baada ya Jeshi la Magereza kuwapima Ukimwi wafungwa na
mahabusu 34,793. Kati yao, wanawake ni 1,451 na wanaume ni 33,342.
Akiwasilisha
bungeni mjini hapa jana taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ukimwi,
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jasmin Bunga, alisema wafungwa
waliokutwa na maambukizi ni 953 (asilimia 2.7), akibainisha kuwa wanaume
ni 818 na wanawake 135.
Alisema
kamati yake pia ilielezwa kuwa jeshi hilo katika mwaka 2015/16
waliwapima wafungwa na mahabusu 8,287 na kati yao, waliokutwa na
maambukizi ya Ukimwi ni 376, sawa na asilimia 4.5.
"Kamati
ilipokea taarifa kuhusu hali ya maambukizi ya VVU magerezani pamoja na
upatikanaji wa kinga na tiba ya magonjwa nyemelezi," alisema na
kufafanua zaidi:
"Katika
mahojiano hayo, kamati ilielezwa kuwa Jeshi la Magereza lina jukumu la
kuhakikisha wafungwa na mahabusu wanapata huduma bora za afya kama
ilivyo kwenye jamii nyingine."
Vilevile,
alieleza kuwa kamati yake ilielezwa uwapo wa msongamano wa wafungwa na
mahabusu unaoathiri huduma bora kwa wafungwa, akibainisha kuwa kwa sasa
kuna wafungwa na mahabusu 39,312 wakati uwezo wa magereza ni kuhifadhi
wafungwa na mahabusu 29,552.
Kutokana
na hiyo, Bunga alisema kamati yake inashauri serikali itumie adhabu
mbadala kwa makosa madogo kwa kuwa kufanya hivyo kutapunguza msongamano,
gharama kwa serikali na uwezekano wa kuambukizana magonjwa ya homa ya
ini, Ukimwi na kifua kikuu.
Alisema
kamati yake pia ilitaka kutolewa elimu ya mara kwa mara ili wafungwa na
mahabusu wapate uelewa namna ya kupambana na janga la Ukimwi pamoja na
wapatiwe chanjo ya kuzuia ugonjwa wa homa hatari ya ini.
"Shughuli
zozote zinazohusu dawa za kulevya na Ukimwi magerezani, uongozi wa
magereza uwahusishe waratibu wa Ukimwi na dawa za kulevya wa mikoa na
wilaya ili kubadilishana uzoefu na elimu," alisema.
Kiongozi
huyo wa kamati pia alisema wamebaini kuna upungufu wa dawa aina ya
Septrine ambazo ni muhimu kwa watu wanaoishi na VVU (WAVIU).
Kutokana
na changamoto hiyo, alisema kamati yake inaishauri serikali kuhakikisha
dawa hizo zinazotumika kupambana na magonjwa nyemelezi, zinapatikana
kwa wingi na ziingizwe katika orodha ya dawa za ARVs ambazo wanapewa
WAVIU ili kufubaza makali ya VVU na kuepusha magonjwa nyemelezi.
Bunga
pia alisema kamati yake imebaini kampeni za mwitikio wa masuala
yanayohusiana na VVU na Ukimwi ni kama zimekufa na hivyo watu sasa
wanafanya ngono zembe bila hofu.
Alisema
ukimya huu umesababisha watu kujisahau na hivyo kufanya ngono zembe,
hali ambayo inaweza kuleta mfumuko mkubwa wa maambukizi mapya ya VVU.
"Kamati
inashauri serikali kuwa na mikakati kuhakikisha kamati za kudhibiti
Ukimwi katika kila ngazi zinafanya kazi ipasavyo," alisema.
0 comments:
Post a Comment