WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka vijana wanaioishi kwenye mikoa ambayo
zao la korosho linastawi wachangamkie kilimo cha zao hilo kwa sababu
lina fursa nyingi.
“Mahitaji
ya korosho ni makubwa duniani, korosho zinatumika mahotelini na kwenye
mikutano mikubwa, zinatumika kwenye ndege, kwa hiyo bei yake lazima iwe
kubwa,” alisema.
Ametoa
wito huo Jumapili, Desemba 31, 2017 wakati akizindua kampeni ya kitaifa
ya upandaji mikorosho bora na mipya milioni 10 msimu wa 2017/2018 mjini
Ruangwa, mkoani Lindi. Kaulimbiu ya kampeni hiyo ni: “Korosho ni dhahabu ya kijani, tuitunze, itutunze”.
Waziri
Mkuu alisema anaamini kuwa kijana yoyote mwenye nguvu ya kufanya kazi
hawezi kushindwa kulima zao hilo kwa sababu halihitaji uangalizi mkubwa.
“Kijana yeyote anaweza kulima zao hili kwa sababu ekari moja ina miche
37 hadi 40. Kuna mtu atashindwa kuangalia miche 37 hadi ikue?” aliuliza.
Waziri
Mkuu alisema kilimo cha korosho ni rahisi lakini pia kilimo cha korosho
ni rafiki wa mazingira, kwani miti ikikua inatunza mazingira na
inasaidia kuleta mvua. Alisema mbali ya mikoa inayolima korosho ya
Lindi, Mtwara, Ruvuma Pwani na Tanga, kuna mikoa mingine ambayo udongo
wake umepimwa na kubainika kuwa zao hilo linaweza kustawi bila shida.
Aliitaja
mikoa hiyo kuwa ni Dodoma, Kigoma, Njombe, Songwe na kuongeza kuwa
mikoa ya Singida na Manyara iko mbioni kukamilisha uchunguzi wake.
“Leo
tumeanza usambazaji wa miche ya bure hapa Ruangwa ambao najua
utafuatiwa na wilaya nyingine hapa nchini. Nimeelezwa kwamba mche wenye
kutoa mazao mengi ni wa kuanzia miaka mitatu hadi saba, kwa umri huu
miche ya korosho inaweza kuchanganywa na mazao mengine kama ambavyo
mtashauriwa na maafisa kilimo ili wakati wa palizi ya hayo mazao, shamba
lako la korosho libakie kuwa safi,” alisema.
Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa, yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka jimboni kwake.
Mapema,
akitoa taarifa ya taarifa ya uzalishaji wa miche ya mikorosho msimu wa
2017/18 mkoani Lindi, Katibu Tawala wa mkoa huo, Bw. Ramadhani Kaswa
alimweleza Waziri Mkuu kwamba katika msimu wa 2016/2017, mkoa huo
uliweka lengo la kuzalisha na kupanda miche 1,000,000 ya mikorosho.
“Hadi
mwisho wa msimu huu, jumla miche 716,532 ilizalishwa na kusambazwa kwa
wakulima sawa na asilimia 71.6 ya lengo lililowekwa. Kati ya hiyo,
Halmashauri ya Kilwa ilizalisha miche 55,000, Halmashauri ya Lindi miche
100,000, Manispaa ya Lindi miche 50,000; Halmashauri ya Liwale miche
106,000; Halmashauri ya Nachingwea miche 227,670 na halmashauri ya
Ruangwa miche 177,862,” alisema.
“Miche
hii iligawanywa kwa wakulima bure ambao walipanda kwenye mashamba yao.
Zoezi la tathmini ya miche iliyokua baada ya kupandwa linaendelea kwenye
halmashauri zote za mkoa,” aliongeza.
Bw.
Kaswa alisema kutofikiwa kwa lengo hilo kumechangiwa na kutopatikana
kwa mahitaji yote ya mbegu na vifaa vya uzalishaji, kuchelewa kwa vifaa,
na mwamko mdogo wa vikundi vya uzalishaji.
Alisema
kwa msimu huu wa 2017/2018, mkoa uliweka lengo la kuzalisha miche ya
mikorosho iliyobebeshwa na isiyobebeshwa 7,132,000. Kati ya hiyo, Wilaya
ya Kilwa walilenga miche 1,122,000, Lindi Vijijini 1,550,000, manispaa
ya Lindi 1,000,000, Liwale miche 450,000, Nachingwea miche 1,810,000 na
Ruangwa miche 1,200,000.
“Hadi
kufikia tarehe 29 Desemba, 2017 tayari miche 4,974,425 ilikuwa
imezalishwa na iko tayari kwa kupandwa kwenye mamlaka za serikali za
mitaa kama ifuatavyo:- Kilwa miche 772,000, Lindi Vijijini 1,160,455,
manispaa ya Lindi 771,440, Liwale miche 266,000, Nachingwea 991,070 na
halmashuri ya Ruangwa imezalisha miche 1,013,460,” alisema.
Sherehe
hizo za uzinduzi wa upandaji miche mipya zilihudhuriwa na wakuu wa
mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na wajumbe wa Bodi ya Korosho
Tanzania (CBT). Wakuu wa Wilaya, baadhi ya Wenyeviti wa Halmashauri na
wataalamu kutoka kituo cha utafiti cha Naliendele walishiriki uzinduzi
huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
0 comments:
Post a Comment