Wanachama
wa chama cha Ushirika cha Uru Kati Mawela, wamemuomba Rais John
Magufuli, kuingilia kati mgogoro wa ardhi wakihofia kufilisiwa shamba
walilopewa na Serikali lenye ukubwa wa hekari 213.
Wasiwasi
huo unatokana na kushindwa kesi waliyoifungua dhidi ya kampuni ya
mwekezaji, Laitolya Tours & Safaris, ambayo imejenga hoteli ya
kitalii ya Kilemakyaro Mountan Lodge ndani ya hekari 27.54.
Hayo
yamejitokeza katika mkutano mkuu maalum wa wanachama ulioitishwa jana
Januari 27, mahsusi kujadili hukumu hiyo iliyotolewa Ijumaa ya Januari
19 na Jaji Benedict Mingwa wa Mahakama Kuu Moshi.
Katika
hukumu hiyo, Jaji Mingwa amesema hekari hizo 27.45 ni mali ya Laitolya
Tours and Safaris na kuutaka ushirika huo kukabidhi hati namba CT10663
ili kampuni imilikishwe hekari hizo 27.54.
Mbali
na kuamuru hati hiyo ikabidhiwe kwa msajili wa hati, lakini Jaji Mingwa
ameamuru pia kuwa wana ushirika hao watalazimika kulipa gharama za kesi
hiyo ya madai namba 10 ya mwaka 2015.
Hata
hivyo, Mrajisi Msaidizi wa vyama vya Ushirika mkoa Kilimanjaro,
Henjewele John, ameliwaambia wanachama hao kuwa mwekezaji huyo amempibu
Rais Magufuli na kwamba atampigia simu.
“Niwaahidi
kwamba tutatumia njia zote kuhakikisha kuwa wananchi wa Uru wanapata
haki yao. Hapa tutamwambia Ushirika leteni hati yenu ya kumiliki na huyu
mwekezaji alete hati zake,”amesema.
“Sasa
hivi nataka niwaambie majumba ya watu yanabomolewa. Si mnaona? Kwa hiyo
huyu mzee wetu amebipi sasa akibipu sisi tutapiga. Zama zimebadilika na
kwa hili tutalifikisha kwa Rais,”amesisitiza.
Mwenyekiti
wa Ushirika huo, Richard Kimaro, amesema wao hawakuwahi kumpa mwekezaji
huyo eneo hilo la ardhi, bali walimkodishia lakini aliwazunguka kwa
kushirikiana na baadhi ya viongozi.
“Katika
kipindi chote cha mkataba tangu 1998 hakuwahi kulipa kodi ya pango
ambayo kwa mujibu wa mkataba ilikuwa Dola 700 za Marekani (sawa na Sh1.6
milioni) kwa mwezi,”alidai mwenyekiti huyo.
Kwa
mujibu wa mwenyekiti huyo, ni kutokana na kutolipa kodi hiyo na
kujimilikisha ardhi yao, walifungua kesi ya madai wakitaka ushirika
ulipwe malimbikizo ya kodi yanayofikia Dola 153,600.
Mbali
na kudai fedha hizo, lakini waliiomba mahakama itamke kuwa mwekezaji
huyo ni mvamizi na ameingia kwa jinai katika shamba lao na pia imuamuru
alipe fidia ya jumla ya Sh80 milioni.
Akizungumza
katika mkutano huo, mmoja wa wanachama wa Ushirika huo, Francis Moshi,
alisema wamekanganyikiwa waliposikia wameshindwa kesi na kudaiwa kuwa
wao ndio walivuruga mkataba.
“Tunajiuliza
hivi ni nani hapa alivuruga mkataba kati yetu na Laitolya ambaye
hakulipa kodi ya pango kwa mujibu wa mkataba? Ulikuwa mkataba wa miaka
10 akaongeza sifuri ukawa miaka 100,”amedai.
Makamu
Mwenyekiti wa Ushirika huo, Emanuel Mushi, alisema kilichojificha ni
kuwa baadhi ya viongozi walishiriki kughushi muhtasari wa vikao
mbalimbali kwa maslahi ya mwekezaji huyo.
Wajumbe
wa mkutano huo waliazimia kwa kauli moja, kwamba bodi ya uongozi ya
chama hicho ikate rufaa kupinga hukumu hiyo na pia ilipeleke suala hilo
ngazi za juu Serikalini kupitia kwa Mrajisi.
Hata
hivyo mkurugenzi wa kampuni hiyo, Joachim Minde alipotafutwa jana,
alisema anawashangaa wanachama hao kufanya mkutano badala ya kukata
rufaa kama hawakuridhika na uamuzi.
“Wao
kama wanataka kwenda kwa Rais sijui Waziri wa Ardhi wao waende. Kama
mimi nina haki yangu si lazima nitalalamika? Wao kama nao wanaona wana
haki walalamikie mahakama,”amesema.
“Huwezi
kulalamika kuwa unamtaka Rais sijui unamtaka Waziri. Hili jambo sio la
leo. Alishakuja Waziri wa Ushirika na pia akaja Waziri wa Ardhi hapa.
Sio jambo geni kabisa,”amesisitiza Minde.
Minde
amedai kuwa kinajitokeza ni kwamba wamekuja baadhi ya viongozi wa
Ushirika ambao ni wageni wanaosumbuliwa na njaa na atafurahi sana kama
siri ya mgogoro mzima ujulikane.
Mkurugenzi
huyo alisema huu ni wakati wa kujua mapato na matumizi ya shamba hilo
na kwamba kwa sasa anajiandaa kufungua kesi nyingine ya madai kwa jinsi
walivyopata hasara tangu 1998.
0 comments:
Post a Comment