Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi imebaini madudu katika utekelezaji wa mkataba
wa uagizaji wa magari 777 kwa ajili ya Jeshi la Polisi yaliyoagizwa kwa
gharama za dola za Marekani milioni 29.77 (Sh. bilioni 66.288).
Kutokana
na hali hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni,
amemwagiza katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Projest Rwegasira,
kuunda kamati maalum ya kuchunguza mkataba wa uagizaji wa magari hayo.
Vilevile,
ameagiza kamati hiyo ambayo itahusisha wataalamu kutoka taasisi
mbalimbali, kupitia upya mkataba ulioingiwa mwaka 2013 kati ya serikali
na Kampuni ya Ashok Leyland inayoingiza magari hayo nchini.
Masauni
aliyabainisha hayo jijini Dar es Salaam jana, muda mfupi baada ya
kufanya ziara ya kukagua magari 53 ya jeshi hilo yaliyotolewa bandarini
kwa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Novemba 26, mwaka jana, huku
naibu waziri huyo akibaini matano yana hitilafu.
Rais
Magufuli alifanya ziara bandarini siku hiyo na kukuta magari hayo 53 ya
Jeshi la Polisi na magari mengine 50 ya kubebea wagonjwa yakiwa yamekaa
hapo tangu Juni, 2016 bila kutoka na kuagiza kutolewa mara moja.
Jana,
Masauni alikuta magari hayo yameshatolewa na kuwekwa katika Chuo cha
Polisi Kurasini huku Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) wakiyafanyia
ukaguzi kabla ya kuyakabidhi kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya ukaguzi
zaidi.
Masauni
pia alitembelea bandarini na kubaini kuwa magari mengine 119 ya Jeshi
la Polisi yameshawasili huku malori yakiwa ni mengi kuliko idadi ya
magari madogo ambayo yanahitajika zaidi kwa shughuli za jeshi hilo.
“Tumeamua
kuunda hii kamati itueleze kitaalamu kwanini magari haya yanakuja
malori zaidi ilhali tuna uhitaji mkubwa wa magari madogo katika vituo
vyetu vya polisi nchini na je, mkataba ulielezaje na kama unafuatwa,”
alisema Masauni.
Kuhusu
hitilafu zilizobainika kwenye baadhi ya magari, Masauni alisema kamati
hiyo ichunguze sababu za magari hayo kuharibika ilhali waliagiza magari
mapya na siyo yaliyotumika.
Naibu
Waziri huyo pia alibainisha kuwa ukaguzi wa awali umebaini moja ya
magari kusomeka limeshatembea zaidi ya kilometa 1,000 na kwamba suala
hilo pia, litapatiwa ufumbuzi kwa kuwa serikali iliagiza magari mapya na
si yaliyotumika.
Masauni
alisema kamati itakayoundwa itahusisha pia wataalamu kutoka Chuo cha
Usafirishaji (NIT) na Temesa, ili kuchunguza kwa kina magari hayo.
Jeshi
la Polisi limekuwa likikumbwa na changamoto za kuwa na utekelezaji
wenye utata wa baadhi ya mikataba yake iliyowahi kuingiwa siku za nyuma,
huku ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya
mwaka 2014/15 ikibainisha kuwa jeshi hilo na Shirika la Umeme (Tanesco)
ni miongoni mwa taasisi zinazoongoza kwa madeni na manunuzi makubwa.
0 comments:
Post a Comment