Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 02 Januari 2018 amekutana na Mwanamuziki Nguza Viking na watoto
wake waliofika Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumshukuru kwa
kupatiwa msamaha wa kuachiwa huru kwake Nguza Viking (Babu Seya) na
Mwanae Papii Nguza (Papii Kocha) waliokuwa wakitumia adhabu ya kifungo
cha maisha jela.
Nguza
Viking na Papii Nguza wakiwa na wana familia wengine Nguza Mbangu na
Francis Nguza wamezungumza na Mhe. Rais Magufuli ambapo wamemshukuru kwa
msamaha alioutoa kwao na kwa wafungwa wengine 61 waliokuwa wamehukumiwa
adhabu ya kifo, na wamemuahidi kuwa raia wema na watachapa kazi kwa
juhudi na maarifa.
“Yaani
sijui nisemaje, hapa nina furaha kubwa sana moyoni mwangu, nilikuwa
naomba sana tangu muda mrefu nikutane nae, nimeomba sana sana, hatimaye
leo nimefanikiwa na nimemwambia namshukuru sana kwa kutusamehe na sasa
nipo tayari kuchapa kazi, Hapa Kazi Tu” amesema Nguza Viking na kuungwa mkono na mwanae Papii Nguza.
Nguza
Viking na wanae wamemuombea Mhe. Rais Magufuli na wameiombea nchi, na
pia msemaji wa familia hii Nguza Mbangu amesema wanajipanga kuendeleza
kazi zao za sanaa.
Kwa
upande wake Mhe. Rais Magufuli amewashukuru kwa kuja kumuona na
kumshukuru lakini amesema shukrani zimwendee Mwenyezi Mungu ambaye ndiye
husamehe.
“Najua
mmekuwa mkihangaika kutaka kuniona, nikaona wacha niwasikilize, hata
hivyo mshukuruni Mwenyezi Mungu ambaye ndiye hutoa msamaha, sasa nendeni
mkachape kazi, na mmtangulize Mungu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Wakati
huo huo, Mhe. Rais Magufuli ametia saini kitabu cha maombolezo na kumpa
pole Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
Mazingira Mhe. Kangi Alphaxard Lugola aliyefiwa na Mkewe Kamishna
Msaidizi wa Polisi Mary Lugola.
Kamishna
Msaidizi wa Polisi Mary Lugola amefariki dunia jana asubuhi tarehe 01
Januari, 2018 katika hospitali ya Rabinisia iliyopo Jijini Dar es Salaam
alikokuwa akipatiwa matibabu na msiba upo Gerezani Railway Club Jijini
Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasilino ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
02 Januari, 2018
0 comments:
Post a Comment