Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 31 Januari, 2018 amezindua mfumo wa uhamiaji mtandao (e-Immigration)
ambao utasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi,
kudhibiti ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali na kuimarisha utoaji wa
huduma za kiuhamiaji kwa raia wa Tanzania na wageni wanaoingia na kuishi
hapa nchini kwa madhumuni mbalimbali.
Uzinduzi
wa mfumo huo umefanyika katika ofisi kuu ya uhamiaji Jijini
Dar es salaam na kuhudhuriwa na Mke wa Rais Mhe. Mama
Janeth Magufuli, Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed
Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Seif Ali Iddi, na Waziri
Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Wengine
ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa
Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu, Spika wa Baraza la Wawakilishi
Mhe. Zubeir Ali Maulid, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, Rais Mstaafu wa
Awamu ya Pili Mhe. Dkt. Ali Hassan Mwinyi na Rais Mstaafu wa Zanzibar
Mhe. Amani Abeid Karume.
Kabla
ya kuzindua mfumo wa uhamiaji mtandao Mhe. Rais Magufuli amekagua
teknolojia iliyotumika katika mfumo huo ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa
alama za vidole na baadaye kupatiwa pasipoti mpya ya kielektronikia (e-Passport) ambayo pia imeanza kutolewa leo.
Pasipoti
mpya za kielektronikia pia zimetolewa kwa viongozi wengine wakuu
wa Serikali, Bunge na Mahakama wa Tanzania Bara na Zanzibar,
waliohudhuria uzinduzi huo.
Mhe.
Rais Magufuli amempongeza Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi
Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Idara ya Uhamiaji kwa
kufanikisha mradi wa kuweka mfumo wa uhamiaji mtandao na kuanza kutoa
pasipoti mpya ya kielektronikia kwa gharama nafuu ya
Shilingi Bilioni 127.2 ikilinganishwa na makadirio yaliyowekwa
awali ya Shilingi Bilioni 400.
“Hapa
tumeokoa fedha nyingi za Watanzania, kuna watu walikuwa wamejiandaa
kutupiga na kuchukua hizo Shilingi Bilioni 400, lakini tukatumia vyombo
vyetu mbalimbali, tukafanya uchunguzi na tumefanikiwa
kutekeleza mradi huu kwa gharama nafuu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha,
kwa kutambua kazi nzuri inayofanywa na idara ya uhamiaji baada
ya kupokea maelekezo yake ya kutakiwa kufanya mabadiliko
makubwa, Mhe. Rais Magufuli ameahidi kutoa Shilingi Bilioni 10 kwa ajili
ya kujenga ofisi ya makao makuu ya idara hiyo Mjini Dodoma.
“Kamishna
Jenerali Dkt. Anna Makakala na timu yako mnafanya kazi nzuri, ndio
maana nimewanunulia nyumba 103 kwa ajili ya wafanyakazi kule Dodoma na
leo nitawapa fedha nyingine Shilingi Bilioni 10 mkajenge ofisi nzuri ya
makao makuu, nyinyi endeleeni kuchapa kazi, endeleeni kukamata wahamiaji
haramu na endeleeni kukusanya mapato vizuri” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mapema
akitoa taarifa ya mfumo wa uhamiaji mtandao, Kamishna Jenerali wa
Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala amesema mfumo huo ni muunganiko wa
mifumo mbalimbali ambayo imesanifiwa kufanya kazi kwa pamoja, kutoa
taarifa kwa watumiaji na wadau wa huduma za kiuhamiaji na kwamba kupitia
mfumo huo idara ya uhamiaji inatarajia kutoa pasipoti za kielektronikia
(e-Passport), viza za kielektronikia (e-Visa), vibali vya ukaazi vya kielektronikia (e-Permit) na udhibiti wa mipaka wa kielektronikia (e-Border Management)
kwa awamu nne hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu 2018, pamoja na kutoa
pasipoti ya kielektronikia ya Afrika Mashariki ya Tanzania.
Balozi
wa Ireland hapa nchini Mhe. Paul Sherlock ameipongeza Tanzania kwa
kufanikisha mradi huu na kueleza kuwa mfumo huu wa uhamiaji mtandao ni
alama muhimu ya Taifa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
31 Januari, 2018
0 comments:
Post a Comment