Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 16 Januari, 2018 amepokea hati za utambulisho za Mabalozi 6
walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Mabalozi
waliowasilisha hati zao za utambulisho ni Balozi wa Nigeria hapa nchini
Mhe. Sahabu Isah Gada, Balozi wa Poland hapa nchini Mhe. Krzysztof
Buzalski, Balozi wa Uturuki hapa nchini Mhe. Ali Davutoglu, Balozi wa
Ufaransa hapa nchini Mhe. Frédéric Clavier, Balozi wa Israel hapa nchini
Mhe. Noah Gal Gendler na Balozi wa Australia hapa nchini Mhe. Alison
Chartres.
Akizungumza
na Mabalozi hao Mhe. Rais Magufuli amewapongeza kwa kuteuliwa
kuziwakilisha nchi zao hapa nchini na ameahidi kuwa Tanzania itaendeleza
na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na nchi
hizo.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa wito kwa Mabalozi hao kutilia mkazo ushirikiano
katika masuala ya kiuchumi yakiwemo kuwahamasisha wafanyabiashara na
wawekezaji wa nchi hizo kuja kufanya biashara na kuwekeza hapa nchini,
hususani katika viwanda, kilimo, utalii na utoaji wa huduma mbalimbali
za kijamii na kwamba Serikali itakuwa tayari wakati wote kujenga
mazingira bora ya kufanikisha biashara na uwekezaji huo.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amewaomba Mabalozi hao kufikisha salamu zake kwa
viongozi wa nchi zao, na kuwakaribisha kuitembelea Tanzania ili
kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
16 Januari, 2018
0 comments:
Post a Comment