Mashahidi
watatu kati ya saba wa upande wa mashtaka wametoa ushahidi wao dhidi ya
mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la
Sugu na katibu wa Chadema wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel
Masonga.
Sugu
na Masonga wanashtakiwa kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya
Rais John Magufuli, wakidaiwa kutoa maneno hayo Desemba 30 mwaka jana
katika mkutano wao wa hadhara walioufanya kwenye viwanja vya Shule ya
Msingi ya Mwenge.
Awali,
Wakili wa Serikali, Joseph Pande aliiambia mahakama hiyo kwamba
wanakusudia kupeleka mashahidi wasiopungua saba pamoja na vielelezo
vitano, huku zikiwasilishwa nyaraka za barua zilizotumika kuombea
mkutano pamoja na barua za kuwaruhusu kufanya mkutano huo.
Mkuu
wa polisi wa Wilaya ya Mbeya, James Chacha alikuwa shahidi wa kwanza
kutoa ushahidi wake jana na aliongozwa na mawakili wa Jamhuri, Joseph
Pande, Baraka Mgaya na Ofmed Mtenga.
Katika
ushahidi wake, Chacha aliieleza mahakama hiyo kwamba yeye ndiye
aliyetoa barua ya viongozi hao kufanya mkutano wao wa hadhara baada ya
kutimiza masharti na kuridhika na maudhui waliyoainisha katika barua ya
maombi hayo.
Alisema
miongoni mwa ajenda walizokusudia kuzungumza katika mkutano huo ni
Mbunge Sugu kuwaeleza shughuli za maendeleo alizozifanya katika utumishi
wake wa ubunge pamoja na kutoa salamu za mwaka mpya.
“Katiba
barua yangu ya kuwaruhusu kufanya mkutano ule, niliwaelekeza kwa
maandishi mambo wanayopaswa kuyazingatia ikiwa ni pamoja kutotumia lugha
ya matusi, kufedhehesha au ya viashiria vyovyote vile vinavyoweza
kuvunja amani na usalama wa nchi,” alidai shahidi huyo.
Shahidi
wa pili, ambaye ni mkazi wa Soweto jijini Mbeya, Boniface Mwaitorola
alidai mahakamani hapo, siku ya tukio alikuwa jirani na viwanja vya
shule hiyo na ilipofika saa 10:00 jioni alisogea eneo hilo kwa lengo la
kumsikiliza mbunge wake.
Alidai
katika mkutano huo awali kabla ya Sugu na Masonga kuwasili eneo la hilo
kulikuwa na shamrashamra za watu na muda mfupi viongozi hao waliwasili
na Masonga ndiye aliyemkaribisha Sugu kuhutubia lakini kabla yake, kuna
maneno aliyotamka Masonga ambayo yalisababisha watu kugawanyika makundi
mawili.
Shahidi
wa tatu, askari polisi anayefanya kazi ofisi ya upelelezi mkoa wa
Mbeya, William Nyamakomage aliieleza mahakama hiyo kwamba siku ya tukio
alikuwa nyumbani kwamba na muda mfupi alipigiwa simu na mkuu wake wa
kazi (Mkuu wa upelelezi mkoa wa Mbeya) akimtaarifu kuhusu kuwepo kwa
mbunge huyo kufanya mkutano wa hadhara hivyo anahitaji kufika eneo hilo
kwa ajili ya shughuli kuangalia usalama na kukusanya ushahidi wa lolote
litakalotokea kama ni la uvunjifu wa amani jambo alililofanya.
Baada
ya shahidi huyo kumaliza kutoa ushahidi wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
mahakama hiyo, Michael Mteite aliiahirisha kesi hadi leo itapoendelea na
upande wa Jamhuri kuwasilisha ushahidi wao na Sugu na Masonga
kurudishwa mahabusu.
0 comments:
Post a Comment