Mbunge
wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ametoka Hospitali ya
Nairobi nchini Kenya leo Jumamosi asubuhi kwenda nchini Ubelgiji kwa
matibabu zaidi ya kuurejesha mwili wake katika hali yake ya kawaida.
Lissu
ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanzania (TLS) ataondoka
saa 2.30 asubuhi ya leo Jumamosi na Ndege ya Shirika la Kenya
akiambatana na mke wake, Alicia.
Lissu
ametoka hospitalini hapo ikiwa baada ya matibabu aliyoyapata tangu
Septemba 7 mwaka jana baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na
watu wasiojulikana kwenye makazi yake Dodoma.
Mwanasiasa
huyo amesindikizwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta na
watoto wake pacha, Augustino na Edward, ndugu zake, viongozi na
wanachama wa Chadema.
"Nawashukuru
sana madaktari wa hapa Nairobi na wale wa Dodoma wakiongozwa na Katibu
Mkuu (wa wizara ya afya Profesa Mpoki Ulisubisya waliookoa maisha
yangu," amesema Lissu kabla ya kupandishwa gari la wagonjwa
"Nakwenda
Ubelgiji kwa matibabu, nikirudi mapambano yanaendelea, nawashukuruni
nyote mlioniombea, nawashukuru Wakenya na serikali yao ambao kwa miezi
minne nikiwa hapa walinipa ulinzi wakati wote."
Akizungumza kwa msisitizo mbele ya wabunge na wanachama wa Chadema waliokuwapo amesema "Chapeni kazi, mimi nitarudi kuendeleza mapambano haya."
Kuhusu
gharama, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji amesema gharama za
safari na matibabu zimegharamikiwa na Chadema na TLS.
Baadhi
ya waliokuwapo hospitalini kumsindikiza Lissu uwanja wa ndege ni kaka
yake Alute Mghwai, mdogo wake, Vinceti Mghwai na ndugu wengine.
Pia, Dk Mashinji, Naibu Makatibu Wakuu, John Mnyika (Bara), Salum Mwalimu (Zanzibar).
Wengine
walikuwapo ni wabuge wa Chadema, Susan Kiwanga (Mlimba) na Godbless
Lema(Arusha Mjini), John Heche (Tarime Vijijini), Rose Kamili (Viti
Maalum), Anna Gideria (Viti Maalum).
Kwa niaba ya familia, Alute amesema "Tunamwomba
Mungu ajalie huko anakokwenda akapate matibabu, kwani alivyokuja hapa
sivyo anavyoondoka na tunawashukuru wananchi wa Tanzania na Kenya kwa
ushirikiano wao."
Mbunge
wa Singida Mashariki, Tundu Lissu akitolewa katika Hospitali ya Nairobi
nchini Kenya kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta kwa
ajili ya safari ya kuelekea nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi.
0 comments:
Post a Comment