Wakati
kampuni hodhi ya rasilimali za reli nchini (Rahco) ikianza utekelezaji
wa kubomoa nyumba zote zilizojengwa ndani ya njia ya reli, zaidi ya
wafanyabiashara 200 wa samaki na dagaa jijini Mwanza hawana pa kwenda
baada ya kubomolewa vibanda vyao.
Hata
hivyo, tofauti na vilio vya baadhi ya wananchi wengine wanaokumbwa na
adha kama hiyo, baadhi ya wafanyabiashara hao walikiri kuvamia eneo hilo
tangu mwaka 1994 baada ya reli hiyo kuacha kufanya kazi.
Kutokana
na hatua hiyo, mfanyabiashara wa samaki eneo la Stesheni na Bandarini,
Maige Wambura aliiomba halmashauri kuwatafutia eneo lingine litakalofaa
kwa biashara ili wajipatie kipato.
“Ni
kweli hatukuwa na eneo maalumu ndio maana tulikuwa hapa tukifanya
biashara zetu, lakini leo (jana) tumebomolewa na hatujaelekezwa tunaenda
wapi,” alisema Wambura.
Wambura
alisema watu wapatao 17 walikuwa na vibanda kwenye njia hiyo na
kulikuwa na wakaanga samaki takriban 67, mamalishe 83 na wauzaji wa
matunda zaidi ya 40.
Ofisa
Mfawidhi wa Rahco, Daimon Mwakaliki alisema ubomoaji huo ni utekelezaji
wa mpango wa Serikali kupisha ujenzi wa reli ya kisasa ya (Standard
Gauge).
Bila
kutaja idadi ya nyumba za watu, taasisi za Serikali na zisizo za
kiserikali, kidini, shule na viwanja vya michezo, zitakazoathirika,
Mwakaliki alisema utekelezaji huo umeanza ikiwa ni siku tatu tangu Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuagiza kuanza ubomoaji huo.
Alisema
watakaobomolewa ni wale waliojenga ndani ya mita 15 kutoka stesheni ya
reli hadi bandarini na kutoka njia kuu ya reli na kuendelea, itakuwa
mita 30.
“Zoezi
hili si la kushtukizwa kwani tulitoa notisi kwa watu wote waliovamia
miezi sita iliyopita, baadhi yao walibomoa wenyewe lakini baadhi
walikaidi ingawa pia juzi tulipita kwenye maeneo yote yatakayobomolewa
kuwatangazia kuanza kuwabomolea,” alisema Mwakaliki.
Bomoabomoa
hiyo imeukumba ukuta wa Uwanja wa Nyamagana, ukuta wa Mamalaka ya
Bandari, kiwanda cha samaki cha Vicky na taasisi nyingine yakiwamo
makanisa na nyumba za kawaida.
Kazi hiyo ya ubomoaji ilidumu kwa saa saba ikifanywa chini ya ulinzi mkali wa polisi waliokuwa waliokuwa na silaha.
0 comments:
Post a Comment