Chama
Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro (KNCU), kimejitwisha jukumu la
kuinusuru Benki ya Ushirika ya KCBL isinyang'anywe leseni na kufungiwa
na Benki Kuu (BoT), kwa kuamua kuuza ekari 581 za Shamba la Lerongo.
KCBL
inakabiliwa na upungufu wa mtaji, tatizo ambalo hualika BoT
kunyang'anya leseni na kufungia benki husika, ikiwamo tano kwa pamoja
mwanzoni mwa mwezi huu.
Aidha,
benki hiyo ambayo inamilikiwa na KNCU kwa asilimia 69, inahitaji kiasi
cha Sh. bilioni tano ili kufikisha mtaji wa Sh. bilioni 6.5 ulioelekezwa
na BoT uwe umefikiwa hadi ifikapo Juni, mwaka huu.
Uamuzi
wa kuuza shamba hilo ulitangazwa jana na Mwenyekiti wa KNCU, Aloyce
Kitau, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkakati wa
kuinusuru benki hiyo isifutiwe leseni.
“Baada
ya kupokea taarifa juu ya upungufu wa mtaji wa kuendesha benki yetu ya
ushirika, wanachama wa KNCU (1984) Ltd, waliridhia kuuza moja ya mali
zake na fedha itakayopatikana iongezwe kwenye mtaji wa benki hiyo ili
ifikie kiasi hitajika cha mtaji kama ilivyoelekezwa na Benki Kuu,”
alisema Kitau.
Shamba la Lerongo lililowekwa sokoni kwa sasa na ambalo bado zabuni yake haijatangazwa hata hivyo, lipo katika wilaya ya Siha.
Kitau
aliwasihi wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro kuendelea kutumia benki hiyo
kwani hadi kufikia jana michakato yote na kibali cha kuuza shamba hilo
ilikua imekamilika, na kwamba KCBL itafikia mtaji husika kama
inavyotakiwa kisheria mapema iwezekanavyo.
Wakati
huo huo, taarifa iliyotolewa kwa umma jana na makamu mwenyekiti wa Bodi
ya Wakurugenzi ya Benki ya KCBL, Tumaini Yarumba ilisema benki hiyo
itatimiza vigezo vyote vya kuwa na mtaji hitajika kufikia Juni.Kwa
mujibu wa Yarumba, Benki Kuu iliitaka KCBL kuhakikisha inaendelea kutoa
huduma kwa wananchi wote wa mkoa wa Kilimanjaro.
Taarifa
hiyo inakwenda sambamba na tangazo la BoT la Januari 9, mwaka huu
linalotaka wananchi kuwa na imani kwa sekta ya kibenki nchini kuwa iko
imara na tayari kuwahudumia Watanzania wote kwa ukaribu.
Akitoa
ufafanuzi kuhusu umiliki wa benki hiyo, Meneja wa KCBL, Joseph Kingazi
alisema benki hiyo ya ushirika ina wanahisa 245 ambao ni Vyama vya
Ushirika wa Mazao (Amcos), Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo
(Saccos) pamoja na watu binafsi.
KCBL
iliyoanzishwa miaka 20 iliyopita, ndiyo benki ya kwanza ya ushirika
nchini kufunguliwa na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na
ndio waanzilishi wa mfumo wa stakabadhi ghalani.
0 comments:
Post a Comment