Kampuni
ya Bharti Airtel inayomiliki kampuni ya Airtel Tanzania, imeeleza
kusikitishwa kwake na taarifa ya kamati iliyoundwa kuchunguza umiliki
wake iliyotolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango juzi.
Taarifa
ya Bharti iliyotolewa jana imeeleza kuwa uwekezaji wake ulifuata na
kuzingatia sheria na taratibu zote za nchi kabla ya baraka za Serikali
ya Tanzania.
Juzi,
Waziri Mpango aliwasilisha kwa Rais John Magufuli taarifa ya kamati
iliyoundwa kuchunguza umiliki wa kampuni ya simu ya Airtel na kueleza
jinsi sheria na taratibu zilivyokiukwa katika ubinafsishaji wake.
Kutokana
na ukiukwaji huo, Dk Mpango alisema Serikali inayomiliki asilimia 40 ya
hisa za kampuni ya Airtel imeamua kufanya mazungumzo na kampuni ya
Airtel inayomiliki asilimia 60 ya hisa ili nchi iweze kupata haki yake.
“Lakini
niwaambie Watanzania yale ambayo tumeyaona ni machafu sana, ni mambo ya
hovyo kabisa, nchi yetu kwa kifupi tuliingizwa mkenge, ni fedha nyingi
zimepotea kwa hiyo sisi katika majadiliano haya lengo letu litakuwa ni
kuhakikisha Watanzania wanapata haki yao” alisema.
Waziri
Mpango aliunda kamati hiyo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais
Magufuli la Desemba 20 mwaka jana wakati akiweka jiwe la msingi katika
jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mjini Dodoma.
Lakini
katika taarifa yake ya jana, Bharti imeonyesha mlolongo wa miamala na
matukio kadhaa wakati wa ubinafsishaji ikidai kuwa hiyo inaweza
ikaonyesha uwazi uliokuwapo.
Mchakato
huo ni ule wa kuanzia kutafutwa kwa mwekezaji ndani ya TTCL kwa ajili
huduma za simu za mkononi mwaka 2001 hadi uuzwaji wa Zain kwenda Airtel.
Taarifa
hiyo inaeleza kuwa katika kila hatua, Serikali ilikuwa ikishirikishwa
na kulikuwa na uwazi mkubwa na matakwa yote ya kisheria yalikuwa
yakifuatwa.
“Miamala
yote ilikuwa ikifanyika chini ya usimamizi wa bodi ya wanahisa wa MSI,
wawakilishi wa Benki ya Dunia, Serikali ya Uingereza, Marekani, Uholanzi
na Ujerumani. Makundi hayo ya watu yalishirikishwa ili kuhakikisha
maadili na misingi ya utawala bora katika kampuni,” inaeleza taarifa
hiyo.
Imemuomba
Waziri Mpango kuipatia matokeo ya kamati hiyo kuhusiana na
ubinafsishaji wake ili kama kuna hoja zozote iweze kuzijibu kwa hoja
kutokana na kumbukumbu za kampuni.
0 comments:
Post a Comment