MWANAMUME
amelazwa katika hospitali moja ya Kaunti ya Kirinyaga Kenya baada ya
kuviziwa na mtoto mmoja wa mtaani akimdai pesa za Sikukuu ya Krismasi
kwa msingi kuwa ndiye "baba mzazi aliyekwepa majukumu ya ulezi".
Mwanamume
huyo kutoka Kijiji cha Kandongu alifumaniwa katika mji wa Ngurubani
mnamo Desemba 25 na alipoulizwa kuhusu pesa za sikukuu, akasema hana.
Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi wa Mwea Mashariki, Kizito Mutoro,
mwanamume huyo alitandikwa kwa kigongo kichwani, akaanguka chini nao
watoto wengine wa mtaani wakaingilia na kumtandika kisawasawa wakimuonya
kuhusu kuhepa majukumu ya ulezi.
Hata
hivyo, mwanamume huyo aliyejitambulisha kama David Muriithi Wachira,
33, alijitetea akisema kuwa alikuwa mwaathiriwa wa utapeli wa vijana hao
wa mitaani ambao mara kwa mara hutekeleza visa kama hizo dhidi ya
wanaume.
“Mimi
sio baba ya mtoto huyo. Sijawahi hata kuzaa nje ya ndoa yangu na
nilishangaa kusikia nikidaiwa Sh10, 000 na kijana ambaye hata sijawahi
kumuona,” amesema Wachira.
Amesema
kuwa yeye alikuwa katika pitapita zake ambapo alisikia amesimamishwa
kwa kushikwa mashati na ndipo hadithi hiyo ikaundwa papo hapo akiitishwa
Sh10, 000.
“Nilishtukia
tu nimezabwa kofi, kisha nikaangukiwa na kigongo kichwani, nikajihisi
nikiishia na nguvu za magoti na mara ya mwisho nakumbuka tu nikianguka
chini,” akasema akiwa katika hospitali ya umma ya Kimbimbi.
Babake mwathiriwa, Nahashon Wachira sasa anamtaka Kizito Mutoro awakamate vijana hao na waadhibiwe.
“Kwa
sasa tunashindwa nini kinaendelea. Polisi wanalea wezi hatari wakisema
kuwa hao ni chokoraa. Hawa wanaoanza na utapeli wa kiwango hiki ndio
kesho watakuwa wamejihami kwa bunduki. Ni lazima hatua ichukuliwe sasa,”
akasema.
Mutoro amesema kuwa maafisa wake wameagizwa watekeleze msako dhidi ya watoto hao wa mitaani.
0 comments:
Post a Comment