Ikiwa
imebaki siku moja kabla ya kuuaga mwaka 2017, mbunge wa Singida
Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ametoa waraka akilaani ukiukwaji wa
haki za binadamu na kuminywa kwa uhuru wa kutoa mawazo.
Waraka
huo alioutoa jana Alhamisi Desemba 28,2017 akiwa katika Hospitali ya
Nairobi nchini Kenya anakopatiwa matibabu tangu Septemba 7,2017
aliposhambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi kwenye makazi yake Area D mjini
Dodoma.
Lissu
pia amezungumzia tukio la kutoweka mwandishi wa habari wa kujitegemea
wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Azory Gwanda ambaye
leo ni siku ya 39 tangu alipotoweka akiwa wilayani Kibiti mkoani Pwani
anakofanyia kazi zake.
“Watanzania
ambao wamekuwa wakitumia uhuru wao wa maoni kutoa mawazo wamekuwa
wakikamatwa na kushtakiwa mahakamani... mwanachama wa Chadema, Ben
Saanane na mwandishi wa Mwananchi (Azory Gwanda) wametoweka na
hawajulikani walipo. Hakuna uchunguzi au taarifa za kutoweka kwao,”
amesema.
Lissu
ambaye pia ni mwanasheria wa Chadema amesema vyombo vya habari
vimekuwa katika wakati mgumu baada ya kukutana na mkono wa sheria,
ikiwamo kufungiwa pale vinapoandika habari zinazotafsiriwa kuwa ni za
kichochezi au uongo.
Kupitia waraka huo alioupa jina ‘Barua kutoka kitanda cha Hospitali ya Nairobi’ amezungumzia pia mambo yaliyojitokeza na yanayoendelea katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Waraka
huo ameutoa siku tatu baada ya kusimama kwa mara ya kwanza tangu
Septemba 7,2017 aliposhambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi.
Amesema
kumekuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu na utawala bora, huku
viongozi wa upinzani na wanaharakati wakikamatwa na kuwekwa mahabusu.
Lissu amesema kutokana na watawala kuwashughulikia wanaowakosoa, uhuru wa kutoa maoni umeminya na mijadala haipo.
“Mikutano
ya kisiasa imezuiwa na polisi, viongozi wanakamatwa, wabunge nikiwemo
mimi (Lissu) tumekamatwa mara nyingi kwa sababu zinazohusu majukumu yetu
ya kazi,” amesema.
Amesema,
‘’Hakuna njia rahisi kufikia uhuru sehemu yoyote na wengi wetu
tutapitia bonde la kivuli cha kifo kabla ya kufikia mlima wa matamanio
yetu.”
Pia,
amevilaumu vyombo vya dola akisema tangu Septemba 7,2017 aliponusurika
kuuawa akiwa eneo lenye ulinzi mpaka sasa hakuna mtuhumiwa hata mmoja
anayeshikiliwa kuhusika na tukio hilo.
Kuhusu
onyo la Serikali kwa viongozi wa dini kutojihusisha na masuala ya
kisiasa lililotolewa Alhamisi Desemba 28,2017 na Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi, Lissu amesema ni mwendelezo wa kuwazuia watu wasitumie
uhuru wao kuzungumza na kukosoa.
0 comments:
Post a Comment