Home » » Kigwangalla ataka Mkataba wa makubaliano

Kigwangalla ataka Mkataba wa makubaliano

Unknown | Monday, May 07, 2018 | 0 comments

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ameagiza uandaliwe mkataba wa makubaliano ya awali (MoU) ya utekelezaji wa mradi wa kuendeleza utalii wa picha katika Pori la Akiba Selous.

Mkataba huo wa makubaliano utahusisha wawekezaji kutoka Jiji la London nchini Uingereza na Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA na  utakapokamilika utasainiwa na pande zote mbili.

Dk. Kigwangalla ametoa agizo hilo juzi ofisini kwake Jijini Dodoma kufuatia maombi yaliyowasilishwa kwake na wawekezaji hao, Eva Sanchez na Nicholas Negre.

Akiwasilisha maombi hayo, Sanchez amesema mradi huo utakuwa wa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA ambao ndio wasimamizi wakuu wa Pori la Akiba Selous utakapoanzishwa mradi huo.

Amesema pamoja na mambo mengine mradi huo wa utalii wa picha pia utasaidia kupiga vita ujangili na kukuza uchumi wa jamii zinazozunguka pori hilo.

Dk. Kigwangalla amewataka wawekezaji hao kuwasilisha andiko la mradi huo, kufanya utafiti wa kina na tathmini ya athari za kimazingira zitakazoweza kujitokeza kutokana na uanzishwaji wa mradi huo.

Amesema kwa sasa Serikali inafanya marekebisho ya Sheria mbalimbali zitakazoiwezesha Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA  kutekelezaji majukumu yake ipasavyo ikiwemo uwekezaji wa aina hiyo kwenye sekta ya Utalii wa Picha na Uwindaji wa Kitalii.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, Dk. James Wakibara amesema mamlaka hiyo itatoa ushirikiano wa kutosha kwa wawekezaji hao ili kutimiza azma ya Serikali ya kushirikisha wadau, watu binafsi na wawekezaji katika kukuza sekta ya utalii nchini.

Pori la akiba Selous ndio hifadhi kubwa kuliko zote nchini ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba takriban 50,000 katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara na Ruvuma. Mwaka 1982, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Uneso) lilitangaza eneo hilo kuwa moja ya eneo la Urithi wa Dunia na kuanza kuhifadhiwa.

Advertisement
Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
Support : Copyright © 2018. AFRICAN NEWS BLOG - All Rights Reserved
Imetengenezwa na Edwin Moshi
Inaendeshwa na AFRICAN NEWS BLOG