Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu, Aprili 23 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi wakati akitoa ufafanuzi wa hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kwa muda sasa kumekuwapo na kelele nyingi kutoka katika maeneo mbalimbali ikiwemo wadau na wasomi kuwa Jiji la Dar es Salaam ramani yake haifuatwi na ndiyo sababu kumekuwa na mafuriko ya mara kwa mara.
Hivi karibuni aliyekuwa waziri katika wizara hiyo, Profesa Anna Tibaijuka alisema ramani hiyo iliachwa na watu kuanza kujenga kiholela na hivyo kusababisha mpangilio mbovu wa kuzuia njia za maji na kusababisha mafuriko mara kwa mara.
“Ni kweli, master plan ya Jiji la Dar es Salaam hatujaipitia kwa muda mrefu, ni kama iliachwa, lakini tumeamua kuachana nayo na kutengeneza master plan mpya na imeshachorwa, lakini kwa sasa inafanyiwa mapitio pale wizarani kwangu,” amesema Lukuvi.
Waziri huyo amesema katika utaratibu wa kawaida, ramani za mipango miji hupitiwa kila baada ya miaka sita, lakini ramani ya Jiji la Dar es Salaam haijapitiwa tangu wakati huo na hivyo Serikali imeachana nayo na kuamua kuanza mpango upya.
Akizungumzia hoja za CAG, Lukuvi alikiri kuwa suala la upimaji na ugawaji wa viwanja haliendi vizuri kama alivyoeleza katika taarifa yake akitaja sababu za ukosefu wa watalamu uliokuwepo.
0 comments:
Post a Comment