Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) limeandaa Mkutano wa 11 wa Baraza ambao utaongozwa na Rais John Magufuli wiki hii.
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Raymond Mbilinyi, alisema jana kuwa mkutano huo unaonyesha dhamira iliyonayo serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli ya kuweka mazingira bora ya kufanya biashara na uwekezaji nchini.
“Mkutano huu wa Baraza ni muhimu sana sekta za umma na binafsi kwani unatoa fursa kwa pande mbili hizi kujadiliana namna bora ya kujenga mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji zaidi kwa manufaa ya Watanzania,” alisema Mbilinyi.
Alisema mkutano utafanyika tayari kukiwa na mafanikio makubwa chini ya awamu ya Tano ambapo viwanda zaidi 3,500 vikiwa vimeshaanzishwa katika kipindi kifupi tu cha uongozi wa Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza.
“Huu utakuwa ni mkutano wake wa pili kuuongoza kama Mwenyekiti wa Baraza tangu achaguliwe kuwa Rais wa Awamu ya Tano. Mkutano wake wa kwanza umeleta mafanikio mengi katika sekta za umma na binafsi,” alisema na kuwa utafanyika Jumapili.
Mbilinyi alisema serikali ya awamu ya tano imesimamia mabadiliko mbalimbali yaliyolenga kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuhamasisha ujenzi wa uchumi wa kati na viwanda.
0 comments:
Post a Comment