China
imeridhia kutoa msaada wa Dola za Marekani Milioni 62 sawa na Shilingi
Bilioni 138.3 za Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha
Usafirishaji hapa nchini.
Balozi
wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke amesema hayo leo tarehe 12 Februari,
2018 muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli na kumkabidhi barua
yenye ujumbe wa Rais wa China Mhe. Xi Jinping, Ikulu Jijini Dar es
Salaam.
Mhe.
Wang Ke ameeleza kuwa msaada huo ni sehemu ya misaada na miradi
mbalimbali ambayo China inaitekeleza hapa nchini Tanzania yenye lengo la
kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati yake na Tanzania.
Kwa
upande wake Mhe. Rais Magufuli amemuomba Mhe. Wang Ke kumfikishia
shukrani zake kwa Rais wa China kwa ujumbe na msaada huo ambao amesema
utasaidia kuimarisha huduma za usafirishaji hapa nchini.
Wakati huo huo,
Mhe. Rais Magufuli amepokea taarifa kutoka kwa viongozi wa Shirika la
Simu Tanzania kuhusu mwelekeo wa shirika hilo baada ya kuanza kutumika
kwa sheria namba 12 ya mwaka 2017 ya Shirika la Simu Tanzania,
iliyolibadili kutoka Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na kuwa Shirika la
Simu Tanzania (TTCL Corporation) kuanzia tarehe 01 Februari, 2018.
Pamoja
na kupokea taarifa hiyo Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Omari Rashid
Nundu kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Corp na Bw. Waziri
Waziri Kindamba kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corp, na amewataka kuchapa
kazi kwa juhudi na kuhakikisha TTCL Corp inaongeza ufanisi, na kutoa
gawio kwa Serikali.
Dkt.
Omari Rashid Nundu na Bw. Waziri Waziri Kindamba wamemshukuru Mhe. Rais
Magufuli kwa uteuzi huo na wamesema TTCL itaendelea kujiimarisha kwa
kupanua huduma za mawasiliano nchini, kuongeza na kuboresha bidhaa
ikiwemo TTCL Pesa, kuzalisha faida zaidi na kuusimamia vizuri mkongo wa
Taifa kwa maslahi na usalama wa nchi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Februari, 2018
0 comments:
Post a Comment