Na Beatrice Lyimo- MAELEZO, DODOMA
Serikali
imesema Kikatiba hakuna mgongano wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Katiba ya Zanzibar unaosababisha ongezeko kubwa la kero za
Muungano na mgongano wa kimamlaka baina ya Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi
bungeni jana mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Wingi
Mhe. Juma Kombo lililohusu mgongano wa Katiba hizo.
Prof
Kabudi alisema kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka
utaratibu mahususi wa kushughulikia tafsiri ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano na utekelezaji wake inayobishaniwa kati ya Serikali ya Jamhuri
ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Hadi
sasa hakuna upande wowote baina ya Serikali hizi mbili ambao unatafsiri
tofauti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano au utekelezaji wake”
“Hivyo
kwa kuzingatia kuwa hakuna mgongano wa Katiba kati ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali
haina sababu ya kuleta mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba ili kuondoa
changamoto hiyo ambayo haipo.” alifafanua Prof Kabudi.
Akizunguzmzia
kuhusu mgongano wa kimamlaka Prof. Kabudi alisema kuwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania anamamlaka yote katika masuala yanayohusu
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha,
akijibu swali la Mbunge wa Korogwe Mjini Mary Chandanda kuhusu
upandishwaji vyeo kwa Mahakimu na Watumishi wa Mahakama, Prof Kabudi
alisema kuwa suala la kupandisha vyeo watumishi wenye sifa stahiki ni
wajibu endelevu kwa Serikali.
“Mahakama
ya Tanzania imekuwa ikichukua hatua kuwapandisha Mahakimu na Watumishi
wa ngazi mbalimbali vyeo kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa kisheria
ikiwa ni pamoja na muda wa utumishi kazini, utendaji kazi, weledi na
maadili pamoja na upatikanaj wa vibali kutoka Idara Kuu ya Utumishi,”
alisema Prof Kabudi.
Hata
hivyo, Prof. Kabudi alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2012/2013 jumla ya
Mahakimu na Wasaidizi wa Sheria wa Majaji 52 walipandishwa vyeo, mwaka
2013/2014 jumla ya watumishi 200 walipandishwa vyeo, mwaka 2014/2015
Mahakimu na Wasaidizi wa Sheria wa Majaji 22 na watumishi 686
walipandishwa vyeo na mwaka 2015/2016 Mahakimu na Wasaidizi wa Sheria 59
na watumishi 447 walipandishwa vyeo.
0 comments:
Post a Comment