Baada
ya mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu na Katibu wa
Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga kuhukumiwa
kifungo cha miezi mitano jela, wakili wao Peter Kibatala amesema
wanakusudia kukata rufaa.
Sugu
na Masonga wamehukumiwa adhabu hiyo leo Februari 26,2018 na Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Michael Mteite.
Wawili
hao wamehukumiwa kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais
John Magufuli, kosa walilotenda kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika
Desemba 30,2017 eneo la Uwanja wa Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.
Kibatala amesema baadaye watatoa taarifa ya nini kinaendelea ila wanakusudia kukata rufaa.
Baada
ya hukumu kutolewa viongozi wa Chadema waliokuwepo mahakamani waliingia
kwenye magari yao na kuelekea katika ofisi za chama hicho Kanda ya
Nyanda za Juu Kusini.
Wakati
wa usomwaji wa hukumu hiyo, nje ya jengo la mahakama ulinzi
uliimarishwa kukiwa na askari waliotanda hadi maeneo ya jirani.
Sugu ni mbunge aliyeweka rekodi ya kupata kura nyingi kuwashinda wabunge wote wa majimbo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Katika uchaguzi huo, Sugu alipata kura 108,566 akiwaacha wapinzani wake kugawana kura 57,690.
Hukumu
imetolewa na hakimu Mteite aliyesikiliza shauri hilo baada ya upande wa
mashtaka na wa utetezi kukamilisha ushahidi Februari 9,2018.
Jamhuri
iliwasilisha mashahidi watano na kielelezo kimoja cha sauti iliyodaiwa
kurekodiwa na shahidi wa tano, Inspekta Joram Magova.
Upande wa utetezi uliwasilisha mashahidi sita wakiwamo Sugu na Masonga waliokana kutamka maneno waliyoshtakiwa kuyatoa.
Washtakiwa
walitetewa na mawakili Sabina Yongo, Boniface Mwabukusi na Hekima
Mwasipu kabla ya kujitoa na kazi hiyo kufanywa na Kibatala.
Kwa
mara ya kwanza, Sugu na Masonga walifikishwa mahakamani Januari 16 na
kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande aliyeeleza
upelelezi ulikuwa umekamilika na walikuwa tayari kuendelea na
usikilizaji.
0 comments:
Post a Comment