WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameuvunja Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza zao la
Kahawa (CDTF) na amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) kuchunguza mwenendo wa mfuko huo tangu ulipoanzishwa.
Ametoa
agizo hilo jana (Jumapili, Januari 14, 2018) wakati akizungumza na
wadau wa zao hilo kwenye kikao cha kujadili maendeleo ya zao la kahawa
alichokiitisha, mjini Dodoma.
Waziri
Mkuu amechukua hatua hiyo baada ya kubaini kwamba uundwaji wa mfuko huo
si wa kisheria bali ni wadau wa zao hilo kwa kushirikiana na Bodi ya
Kahawa Tanzania (TCB).
“Wakati
Serikali inapambana kupunguza makato ya hovyo kwa wakulima, kumbe huku
kuna chombo cha kuwachukulia fedha wakulima hii haikubaliki.”
Pia
aliagiza kufungwa kwa ofisi za CDTF ili kupisha uchunguzi na baada ya
CAG kukamilisha uchunguzi na kukabidhi ripoti, kazi zote zilizokuwa
zinafanywa na mfuko huo zitafanywa na Bodi ya Kahawa.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu ameongeza kuwa majukumu ya kuundwa kwa mfuko huo
yanaingiliana na yale ya Bodi ya Kahawa, ambayo ni pamoja na kufuatilia
maendeleo ya zao hilo, hivyo hakuna haja ya kuwa vyombo viwili
vinavyofanya kazi moja.
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu amepiga marufuku wanunuzi wa kahawa kwenda kununua kwa
wanavijiji na badala yake kahawa yote itauzwa kwa njia ya minada.
“Kahawa
itauzwa katika minada tu na utaratibu wa kutoa vibali kwa wanunuzi wa
kahawa kwenda kununua kwa wananchi vijijini marufuku kuanzia sasa, kama
kuna watu wamepeleka fedha zao wazirudishe kwani hazitafanya kazi.”
Amesema
Wakuu wa Mikoa na Wilaya wasimamie uuzwaji wa zao hilo na kuwachukulia
hatua wote watakaokutwa wananunua kahawa kwa wakulima. “Anayetaka kahawa
akanunue mnadani na si kwa wanavijiji lengo ni kuhakikisha mkulima
anapata tija.”
Pia
ameziagiza halmashauri zote zinazolima kahawa nchini kuanzisha vitalu
vya miche ya kahawa na kisha kuigawa bure kwa wakulima, pia Maofiza
Kilimo wawaelimishe walkulima wote wenye miti mikongwe waanzisha
mashamba mapya.
Kuhusu
suala la utafiti wa zao hilo, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo
itumie vyuo vyake vya kilimo ianzishe vituo vyake vya utafiti
vitakavyofanya kazi ya utafiti wa zao hilo.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. Joseph
Kakunda amesema watahakikisha maagizo hayo yanafanyiwa kazi, ambapo
aliwaagiza Wakuu wa mikoa yote 16 inayolima kahawa pamoja na wakuu wa
wilaya wake 52 wahakikishe wanafuta mara moja vibali vya ununuzi wa
kahawa katika vyanzo vyao vya mapato.
Kikao
hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina mjini Dodoma kilihudhuliwa
na Waziri wa Kilimo Dkt. Chales Tizeba, Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwekezaji Bw. Charles Mwijage, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais-TAMISEMI, Bw. Kakunda.
Wengine
ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,, Bibi Maimuna Tarishi, Katibu Mkuu
Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe, Wakuu wa mikoa 16 wanaolima
kahawa na wakuu wa wilaya,Mrajis wa Vyama vya Ushirika Nchini, Dkt.
Tito Haule, Makatibu tawala wa mikoa inayolima kahawa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa na wajumbe wa bodi hiyo,,Mkurugenzi wa bodi ya Kahawa Tanzania, Wakurugenzi wa Halmashauri,
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
0 comments:
Post a Comment