WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amebaini madudu kwenye Vyama Vikuu vya Ushirika
vya Mbinga (MBICU na MBIFACU) na kuagiza uchunguzi ufanyike kuanzia leo.
“Nikiondoka
hapa jukwaani, viongozi wote wa zamani na wa sasa waripoti kwa Mkuu wa
Wilaya, na OCD hakikisha ofisi za chama hazifunguliwi hadi kesho asubuhi
(leo) kazi itakapoanza, ili wasije kubadilisha nyaraka kwenye ofisi
yao. Timu yangu ya uchunguzi iko hapa Mbinga, kesho waende wote kwenye
ofisi hizo,” alisema huku akishangiliwa na wananchi.
Ametoa
agizo hilo Ijumaa, Januari 5, 2018 wakati akiwahutubia maelfu ya wakazi
wa mji wa Mbinga, kwenye viwanja vya CCM, mjini Mbinga.
“Natambua
kuwa MBICU ilishakufa ikiwa na madeni makubwa na mkaunda tena MBIFACU,
ambayo nayo inasuasua, lakini viongozi wote hawa watafutwe, waje waonane
wa timu yangu na waeleze fedha za chama zimeenda wapi na kama
walizikopea zilifanya nini,” alisisitiza.
Alisema
timu hiyo ya uchunguzi itakiangalia chama hicho na kukifumua chote, na
wote wakaobainika kuhusika watachukuliwa hatua za kinidhamu. “Tunataka
MBICU na madeni yenu yaliyoko kwa Msajili wa HAZINA yajulikane, tunataka
turudishe hoteli yetu, mashamba yetu na majengo yetu,” alisema.
Waziri
Mkuu aliwaeleza wananchi hao kuwa Serikali imeamua kuboresha ufanisi
katika mazao matano ya biashara ambayo ni pamba, kahawa, chai, korosho
na tumbaku kwa sababu yanaliingizia Taifa fedha za kigeni.
“Mazao
haya tutayasimamia kuanzia kilimo hadi uvunaji na utafutaji wa masoko.
Nimeshafuatilia mazao ya korosho, tumbaku na pamba. Na sasa nimeanza na
zao la kahawa na nimeamua kuanzia huku Mbinga,” alisema.
Alisema
Serikali imedhamiria kuimarisha zao la kahawa katika mikoa yote
inayolima zao ikiwemo Ruvuma, Mbeya, Kagera, Kigoma na maeneo mengine.
“Na
nikimaliza ziara hii, nimeitisha kikao cha wadau wa zao la kahawa mjini
Dodoma ifikapo Januari 14, 2018. Nimewaita Wakuu wa Mikoa, wakuu wa
wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa ushirika, Maafisa kilimo na
wadau wote kutoka mikoa yote inayolima kahawa hapa nchini, tukutane na
kupeana maelekezo juu ya usimamizi wa zao hili,” alisema.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu ameagiza kwamba kuanzia msimu ujao, zao la
kahawa litauzwa kwa mnada chini ya mfumo wa ushirika. “Kuanzia msimu
ujao, kahwa yote utauzwa kwa mnada, mnunuzi yeyote akitaka kununua
kahawa aende kwenye mnada, tukikukuta mtu ananua kahawa kwa mkulima
tutamkamata,” alisema na kuamsha shangwe kwa wananchi hao.
Alisema
kuna watu wamekuwa wanapita na kununua kahawa kwa mfumo wa ‘magoma’
ambapo huwalaghai wakulima kwa kuwapa noti chache za sh. 10,000. “Huu
mfumo wa magoma ni wa kuwaibia wananchi, hatutaki tena kuuona. Hakuna
tena magoma hapa Mbinga,” alisisitiza.
“Bei
ya mnada ndiyo fedha ya mkulima na sasa, Serikali tumeondoa tozo 17
kwenye zao hili kwa sababu tunataka tuone mkulima afaidike na zao hili,”
alisema.
Waziri
Mkuu anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma kwa kutembelea
wilaya ya Nyasa ambako atazungumza na watumishi na madiwani, ataweka
jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, atakuwa mgeni rasmi
kwenye tamasha la utalii na pia kuhutubia mkutano wa hadhara.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
0 comments:
Post a Comment