Mahakama
ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Bukoba, imewahukumu kifungo cha
maisha watu watatu, baada ya kuwatia hatiani kwa makosa mawili, likiwamo
la kuchoma moto kanisa.
Kanisa lililochomwa moto na watu hao ni la Evangelical Assemblies of God (EAGT) mjini Bukoba mkoani Kagera.
Waliotiwa hatiani na Hakimu wa Mahakama hiyo, Charles Oisso ni Rashid Athuman, Ngesella Ismail na Allyu Dauda Hessein.
Hakimu
Oisso alisema kuwa watu hao wametiwa hatiani kwa makosa mawili, la
kwanza ni kula njama za kutenda kosa walilohukumiwa kifungo cha miaka
saba, na la pili ni kutenda kosa la kuchoma kanisa la Evangelical
Assemblies of God (EAGT) lililoko mtaa wa Omukibeta Kata ya Kibeta
katika Manispaa ya Bukoba.
Alisema kuwa aliwatia hatiani kutokana na washtakiwa hao kuonyesha vitendo vya chuki dhidi ya dini nyingine.
Hakimu Oisso alisema kuwa maeneo ya ibada inabidi yawe salama, maana siyo sehemu ya kujengea watu hofu.
Kwa
upande wake, Mwanasheria wa Serikali, Haruna Shomari, awali aliiomba
mahakama hiyo kuwapa adhabu kali washtakiwa hao, ili kukomesha vitendo
vya aina hiyo, ambavyo alisema vinajenga hofu kwa jamii.
Mwaka
2015, washtakiwa hao walikamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za
kuchoma moto kanisa hilo ambalo liliteketea pamoja na vitu
vilivyokuwamo, na kufikishwa mahakamani mwaka huo.
0 comments:
Post a Comment