Mamlaka
ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), imeeleza kuwa
ina mpango wa kufunga mfumo wa kuratibu mwenendo wa mabasi (VTS), katika
mabasi yote ili kuweza kukusanya taarifa za mwenendo wa mabasi
yanayosafirisha abiria kwenda mikoa mbali mbali hapa nchini.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Sumatra, Williard Ngewe, alieleza hayo jana, Jumapili,
Januari 7, 2018, jijini Mbeya wakati wa mkutano wa kutoa elimu kwa wadau
wa usafirishaji mkoani humo juu ya sheria mpya ya usimamizi wa usafiri
wa mabasi.
Mkurugenzi
Ngewe aliongeza kuwa wameamua kufunga mfumo huo ili kupima mwenendo wa
mabasi ya mikoani na kisha baadae kuruhusu mabasi hayo yawe yanafanya
safari zake muda wowote (mchana na usiku) ili kuongeza tija katika sekta
ya usafiri nchini.
Alisema
mfumo huo unasaidia mamlaka hizo mbili kutambua matatizo kwenye mabasi
pindi inapotokea na hivyo hatua za haraka kuchukuliwa ili kudhibiti
madhara.
“Kuna
kitufe maalumu kwenye mfumo huo ambacho dereva anapopata tatizo,
ikiwamo basi kutekwa, kupata ajali ama basi linapoharibika katika sehemu
ambayo inayotakiwa ulinzi, anabonyeza kisha taarifa zinafika Sumatra na
Polisi…(halafu) tunachukua hatua za haraka kuokoa,” alisema Ngewe.
Aliongeza
kuwa lengo kubwa la kufunga mfumo huo kwenye mabasi ya abiria yaendayo
mikoani, ni katika kuhakikisha kuwa wanapunguza ajali kwa kuratibu
mwenendo wa madereva, kondakta pamoja na usalama mzima wa basi
linapokuwa safarini.
Kwa
upande wake, Meneja wa Huduma za Sheria wa Sumatra, Leticia Mutaki,
alisema kwa mujibu wa sheria mpya ya usafirishaji, miongoni mwa makosa
yaliyoainishwa kuwa yanaweza kulifungia basi ni kuchezea mfumo huo wa
VTS.
Meneja
Mutaki, alisema kutokana na malalamiko ya wadau na maoni mbalimbali
yaliyotolewa, sheria hiyo imeshafanyiwa marekebisho na kwamba makosa ya
mmiliki na dereva yametofautishwa na kila mmoja wao ana nafasi yake
katika basi husika.
Alisema
dereva pamoja na kondakta watawajibika kwa vitendo vyote vya utovu wa
nidhamu wakati wakiendelea na safari ikiwamo kuonyesha video ambazo zipo
kinyume cha maadili zikiwamo za watu wanaoonekana wakiwa watupu.
“Lengo
la kuanzisha mfumo huu ni kuongeza tija kwenye sekta yetu hii ya
usafirishaji, sasa sheria imeweka wazi kuwa endapo mfumo huo utabainika
kuwa umechezewa, basi husika litafungiwa kufanya kazi kwa siku 30,”
alisema Mutaki.
0 comments:
Post a Comment