Kocha
Mkuu mpya wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre, amekishuhudia kikosi
chake kikiibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Singida United katika
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.
Katika
ushindi huo uliochangiwa na Mganda Emmanuel Okwi aliyetokea benchi na
kutupia mawili katika kipindi cha pili, Simba ilicheza kwa kujiamini
zaidi ya wageni hao.
Lechantre,
ambaye alitangazwa rasmi jana kuwa Kocha Mkuu wa Simba, ni wa kiwango
cha juu, na haijawahi kutokea kwa klabu za hapa nchini kunasa kocha wa
kiwango hicho katika kipindi cha hivi karibuni, imefahamika.
Lechantre
ambaye aliwasili nchini juzi usiku na kuanza mazungumzo na viongozi wa
klabu hiyo ambayo jana mchana yalifikia tamati baada ya kukubaliana,
sasa anazima tetesi za majina kibao ya makocha waliokuwa wakihusishwa
kupewa mikoba ya Mcameroon Joseph Omog.
Moja
ya sifa kubwa ya kocha huyo katika kipindi cha hivi karibuni ni pamoja
na kuinoa timu ya Taifa ya Congo mwaka 2016, ambayo imekata tiketi ya
kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika Urusi baadaye
mwaka huu, na sasa amepewa mikoba ya kuiongoza Simba baada ya viongozi
wa klabu hiyo kuamua kuachana na Mbrazil Fabio Lopez, aliyeko nchini
tangu Jumanne.
Mkuu
wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, jana alisema
Lechantre atasaidiwa na Mrundi Masoud Djuma, ambaye alikuwa akikaimu
nafasi hiyo baada ya kuondoka kwa Omog.
Manara
alisema Lechantre amefuatana na kocha wa viungo, Mohammed Aymen, raia
wa Morocco na baada ya kufikia makubaliano, wanatarajia kukamilisha
taratibu za kupata kibali na hatimaye Mfaransa huyo aweze kuanza kazi
yake mapema.
Sifa
nyingine ya Lechantre, ni kwamba analifahamu vema soka la Afrika, kwani
aliwahi kuiongoza Cameroon kuchukua ubingwa wa Afrika mwaka 2000 huku
klabu alizowahi kuzifundisha ni pamoja na Al Ittihad ya Libya, Al Arabi
(Qatar), CS Sfaxien na Club Africaine zote za Tunisia.
Mbali
na kuiongoza Simba kuwania taji la Ligi Kuu Tanzania Bara ambalo
linashikiliwa na Yanga, Mfaransa huyo atatakiwa kuhakikisha ‘Wekundu wa
Msimbazi’ hao wanaodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni
ya SportPesa, wanafanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa ya Kombe
la Shirikisho Afrika yatakayoanza mapema mwezi ujao.
0 comments:
Post a Comment