Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 22 Januari, 2018 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi
6 walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Mabalozi
waliowasilisha hati zao ni Mhe. Konstantinos Moatsos – Balozi wa
Ugiriki hapa nchini mwenye makazi yake Nairobi nchini Kenya, Mhe. Fafre
Camara – Balozi wa Mali hapa nchini mwenye makazi yake Addis Ababa
nchini Ethiopia na Mhe. Dina Mufti Sid – Balozi wa Ethiopia hapa nchini
mwenye makazi yake Nairobi nchini Kenya.
Wengine
ni Mhe. Elizabeth Taylor – Balozi wa Colombia hapa nchini mwenye makazi
yake Nairobi nchini Kenya, Mhe. Martin Gomez Bustillo – Balozi wa
Argentina hapa nchini mwenye makazi yake Nairobi nchini Kenya na Mhe.
Uriel Norman R. Garibay – Balozi wa Ufilipino mwenye makazi yake Nairobi
nchini Kenya.
Mhe.
Rais Magufuli amewapongeza Mabalozi wote kwa kuteuliwa kuziwakilisha
nchi zao hapa nchini na ameahidi kuwapa ushirikiano utakaowezesha
uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi zao kukua zaidi.
Mhe.
Rais Magufuli amewahakikishia kuwa Tanzania inatambua uwepo wa fursa
mbalimbali za kibiashara na kiuchumi katika nchi hizo pamoja na ujuzi na
uzoefu katika nyanja mbalimbali, na kwamba ni matarajio yake kuwa ujio
wao utasaidia kuongeza manufaa ya kiuchumi na kubadilishana uzoefu.
Pia
Mhe. Rais Magufuli amewaomba Mabalozi hao kufikisha salamu zake kwa
viongozi wa nchi zao na amewakaribisha kutembelea Tanzania.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
22 Januari, 2018
0 comments:
Post a Comment