Home » » Madiwani waivamia shule na kumfukuza Mwalimu Mkuu na kuifunga Ofisi yake

Madiwani waivamia shule na kumfukuza Mwalimu Mkuu na kuifunga Ofisi yake

Unknown | Thursday, January 11, 2018 | 0 comments
KIZAAZAA kilitokea katika shule ya sekondari ya wavulana ya Friends Kamusinga kaunti ya Bungoma, madiwani walipowaongoza wakazi kuivamia na kumfukuza mwalimu mkuu mpya aliyeanza kazi wiki iliyopita na kufunga ofisi yake

Madiwani watatu walimfurusha Bw Alex Kariuki Maina kutoka shule hiyo iliyoko eneobunge la Kimilili na kuitaka Tume ya Huduma ya Walimu (TSC) kumtuma kufanya kazi kwingine. Shughuli za masomo na usajili wa wanafunzi wa kidato cha kwanza zilisimamishwa kwa muda viongozi hao walipovamia shule hiyo wakiandamana na wakazi.

Wakiongozwa na diwani wa wadi ya Kibingei Bw Aggrey Mulongo, diwani wa Soysambu/ Mitua Stephen Wafula na diwani maalumu Luke Opwora wakazi walisema hawatamruhusu Bw Kariuki katika shule hiyo.
Bw Maina  alihamishiwa shule hiyo kutoka shule ya wavulana ya Oloolaiser kaunti ya Narok kuchukua nafasi ya Edwin Namachanja ambaye alihamishiwa shule ya wavulana ya Maranda kaunti ya Siaya.
TSC iliwahamisha walimu wakuu zaidi ya 500. Bw Mulongo alimlaumu Bw Maina kwa kusimamia vibaya shule ya Oloolaiser. “Hatutaki ukabila, tunachotaka TSC ifanye ni kuchukua mfanyakazi wao na kumtuma mahali pengine, hawezi kufanya kazi katika shule hii, hatutakubali mtu aliyeshindwa kwingine kusimamia shule kubwa kama hii,” alisema.
Juhudi za maafisa wa polisi waliokuwa na silaha kuingilia kati hazikuzaa matunda na mwalimu huyo akatimuliwa na madiwani hao na wakazi.
Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati na maafisa wa vyama vya walimu wamekuwa msitari wa mbele kuitaka TSC na kaimu waziri wa elimu Fred Matiang’i kubatilisha uhamisho wa walimu wakuu kaunti hiyo.
Akihutubia walimu wakuu zaidi ya 300 katika shule ya Bungoma Ijumaa wiki jana, Bw Wangamati alisema hatakubali shule zinazofanya vyema eneo hilo kusimamiwa vibaya.
“Hatuwezi kukubali mwalimu mkuu kutoka shule iliyo na alama za wastani 5.9 kusimamia shule iliyo na alama za wastani 9.2, wacha walimu wakuu hao wahamishiwe shule wanazoweza kuongoza,” alisema Bw Wangamati.
Alisema walimu wakuu hao wakiruhusiwa kusimamia shule hizo, zitafanya vibaya kwenye mitihani.
Kamanda wa polisi kaunti ya Bungoma Charles Munyoli alisema hali ya kawaida ilirejea katika shule hiyo na mwalimu mkuu huyo akarejea kazini.
Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
Support : Copyright © 2018. AFRICAN NEWS BLOG - All Rights Reserved
Imetengenezwa na Edwin Moshi
Inaendeshwa na AFRICAN NEWS BLOG