Mahakama
ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, imemhukumu mkazi wa mtaa wa barabara
ya Mbutu, mjini hapa, Mohamed Ahmed (54) kifungo cha miaka mitatu jela
baada ya kutiwa hatiani kwa kumtishia na kumtolea lugha ya matusi Mkuu
wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo.
Mwendesha
Mashtaka wa Polisi, Elimajidi Kweyamba, alidai mahakamani hapo kwamba
mshitakiwa, alitenda kosa hilo Januari 09, mwaka huu, saa 1:05 usiku
katika maeneo ya barabara kuu ya lami ya Igunga mjini.
Alidai kuwa mshitakiwa huyo alimtolea lugha ya matusi Mwaipopo wakati akitekeleza majukumu yake.
Mbele
ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Igunga, Ajali Milanzi, Kweyamba
alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo wakati mkuu wa wilaya
akitekeleza agizo la upandaji miti kama lilivyotolewa maelekezo na
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassani.
Aidha,
mwendesha mashtaka alidai kwamba katika kosa la pili, muda huo huo na
tarehe hiyo hiyo, mshitakiwa akiwa na nia ovu, alimtishia maisha kwa
maneno Mkuu wa Wilaya kuwa atamwonyesha na atahakikisha anahama Igunga
kwa kumfanyia kitu kibaya.
Hata hivyo, baada ya kusomewa mashitaka yote mawili, mshtakiwa huyo alikiri kutenda makosa hayo.
Kabla
ya kutoa hukumu, Hakimu Milanzi alisema kwa kuwa mshtakiwa amekiri
mwenyewe makosa, atatumikia adhabu ya kifungo cha miaka mitatu gerezani,
mwaka mmoja kwa kosa la kwanza na miwili kwa kosa la pili.
0 comments:
Post a Comment