MWENYEKITI
wa Kamati ya Amani Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Shehe wa mkoa
huo, Alhad Mussa Salum amewataka viongozi wa kidini kuacha siasa za
chuki dhidi ya viongozi wa kitaifa katika majukwaa yao ya ibada.
Akizungumza
Dar es Salaam jana, Shehe Alhad alisema siku za hivi karibuni
kumejitokeza baadhi ya viongozi wa kidini kutoa kauli mbalimbali zenye
lengo la kuwachonganisha wananchi na viongozi wakuu wa kitaifa akiwemo
Rais John Magufuli, suala alilodai halina budi kukemewa kwa kuwa sio
mahali pake.
Alisema
viongozi wa kidini wana nafasi kubwa katika jamii na kutokana na nafasi
hizo pia wanazo fursa mbalimbali za kuwasilisha mawazo yao bila tatizo
lolote kwa kufuata utaratibu unaoeleweka, ila siyo kwa kusimama mbele ya
waumini wao wakati wa ibada na kutoa kauli za kisiasa zinazolenga
kuvuruga amani.
“Sisi
viongozi wa kidini tumepewa wigo mkubwa sana wa kufikisha mawazo yetu,
siyo kwamba tunakatazwa kuikosoa serikali kwa jambo lolote…hapana, hiyo
ni haki yetu ila hapa ni utaratibu upi tunautumia kufikisha kile
tunachokiona hakiendi sawa,” alisema Shehe Alhad.
Alisema
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli imefanya kazi nzuri na
kubwa ikiwemo ya kukomesha ufisadi, rushwa, unyonyaji, nidhamu kazini,
kudhibiti mapato na mengine, huku ikipiga hatua katika kuongeza kasi ya
maendeleo, jambo alilosema ni vyema kama litapokewa kama sehemu ya
kujivunia kwa viongozi hao na taifa kwa ujumla.
Alisema
tangu serikali hiyo iingie madarakani miaka miwili iliyopita, Rais
Magufuli pamoja na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa, wamekuwa mstari wa mbele kutembelea makanisa mbalimbali na
misikiti na kuzungumza na waumini pamoja na viongozi wao, na kuhoji
iweje sasa kwa viongozi hao wanageuka tena na kuanza kuwavuruga.
“Utaratibu
sahihi upo na wa nidhamu kwa viongozi wetu ndiyo pekee unaowezesha
kulinda amani na utulivu kwa taifa hili, lakini siyo kwa kukosoana
kwenye nia ya kuchochea waumini wachukie viongozi wao pasipo sababu, leo
kiongozi wa dini anasimama na kukosoa, kesho msemaji wa serikali
akisimama na kujibu mwisho wa siku linakuwa siyo jambo la busara,
kikubwa ni kwa viongozi wenzangu wa dini kuwa na staha,” aliongeza.
Aidha,
kuelekea kuukaribisha mwaka mpya wa 2018, Shehe Alhad amewaomba
Watanzania wote pasina kujali itikadi zao za kidini, kuzidi kuliombea
Taifa ili lizidi kwenda katika njia sahihi kama ambavyo dalili
zimejionesha ndani ya kipindi hiki cha Sikukuu ya Krismasi na katika
miaka miwili chini ya Rais Magufuli. Alisema ushirikiano baina ya
wananchi na viongozi wao wa ngazi zote ndiyo jambo pekee
litakalowasaidia kuvuka kutoka sehemu moja kwenda nyingine katika njia
sahihi za mafanikio.
0 comments:
Post a Comment