Home » » Polisi aliyemuua bosi wake kwa Risasi akamatwa

Polisi aliyemuua bosi wake kwa Risasi akamatwa

Unknown | Friday, December 29, 2017 | 0 comments
POLISI aliyemuua mkubwa wake kwa kumpiga risasi katika kaunti ya Makueni nchini kenya Jumatano usiku alikamatwa Alhamisi katika eneo la Kwa Kanzi katika kaunti hiyo

Kamanda wa polisi kaunti ya Makueni Joseph Napeiyan alisema Bw Friday Barasa, ambaye pia aliwajeruhi wenzake wawili katika kisa hicho, alikamatwa alipokuwa akitoroka.

“Maafisa wetu wamemkamata katika eneo la Kwa Kanzi baada ya kupashwa habari na umma. Afisa huyo muuaji ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria baada ya uchunguzi kukamilishwa,” akasema.
Bw Barasa, mwenye cheo cha Konstebo, alitoroka baada ya kumuua Naibu Afisa Msimamizi (OCS) wa kituo cha polisi cha Makueni Dennis Wanjala Jumatano usiku. Vile vile, aliwajeruhi maafisa wengine wawili katika makabiliano hayo.
Maafisa wa polisi katika kituo hicho walisema Barasa alitekeleza uhalifu huo kwa kutumia bunduki aina ya AK47. Haijulikana ni nini kilimfanya awashambulie wenzake.
Awali, Bw Napeiyan alikuwa amewaomba wakazi kushirikiana na polisi katika juhudi za kumkamata polisi huyo baada ya kupashwa habari kwamba alionekana eneo la Kisingo akikaribia mji wa Makindu.
“Aliabiri matatu katika kituo cha kibiashara cha Mbuvo na akashuka katika eneo la Kisingo na kupanda bodaboda kuelekea nyuma upande wa Wote,” akasema.
“Tuna hofu kwamba jamaa huyu anaweza kuanza kuwahangaisha waendesha magari au kuwaibia wakazi,” Bw Napeiyan akasema.
Jumatano, maafisa ambao wamekuwa wakifanya kazi na mshukiwa walisema afisa huyo, ambaye alikuwa akifanya kazi katika afisi ya kupokea matukio alionekana kuchanganyikiwa siku ya Jumatano huku akisikika akisema kuwa alitaka kutekeleza mauaji.
Baada ya Bw Wanjala kupashwa habari hiyo, yeye na maafisa wengine wawili walielekea katika afisi hiyo kutaka kujua ni kwa nini Barasa alikitoa matamshi hayo.
“Alipowaona maafisa hao Barasa aliwashambulia kwa risasi na kumuua naibu OCS huyo na kuwajeruhi wenzake wawili. Alitoweka na bunduki hiyo baada ya kutekeleza uhalifu huo,” akasema afisa mmoja wa cheo cha juu katika eneo hilo.
Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
Support : Copyright © 2018. AFRICAN NEWS BLOG - All Rights Reserved
Imetengenezwa na Edwin Moshi
Inaendeshwa na AFRICAN NEWS BLOG