Mwendesha
bodaboda maarufu mpaka wa Sirari na Isebania, Kenya, Kiongera Nchagwa
(27) mkazi wa Kijiji cha Gwitiryo, Tarime, Mara anasakwa na Polisi wa
pande zote mbili, akituhumiwa kumuua mwenzake, Jeremia Omera (22) kwa
kumchoma kwa kisu kifuani.
Mwenyekiti
wa Haki za Binadamu Wilaya ya Kurya West ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Wafanyabiashara wa Isebania, Peter Masaithe alieleza tukio hilo
linatokana na ugomvi wa kunyang’anyana mizigo ya abiria aliyetaka kuvuka
mpaka kuingia nchini akitokea Nairobi.
“Tukio
hilo la mwendesha bodaboda Kiongera Mosaisi ambaye ni Mtanzania la
kumchoma kisu kifuani mwenzake, Jeremia Omera Mgusuhi lilitokea Jumamosi
asubuhi saa 1 katika stendi ya mabasi ya Nairobi, Isebania lililokuwa
na abiria kutoka Tanzania,” alisema.
“Walianza
kunyang’anyana mzigo wa abiria aliyeshuka basi la The Guardian akivuka
kwenda Tanzania. Kila mmoja alidaka huo mzigo hivyo ugomvi ukatokea
ambapo Kiongera alijihami kwa kisu na kumchoma kifuani Jeremia na
akatokwa damu nyingi hali iliyopelekea kifo chake na Kiongera akatoroka
kwa kutumia pikipiki yake na kuingia Tanzania,” alisema.
Masaithe
alikemea bodaboda kutembea na visu, kunywa pombe za viroba ambavyo
baada ya kupigwa marufuku sasa vimehamia Isebania hali inayochangia
uhalifu na kuziomba serikali za nchi hizo mbili kuchukua hatua kali
ukiwemo msako wa viroba na bangi ili kuokoa vijana.
Polisi
wa Isebania wamethibitisha kifo cha Jeremia na wamewasiliana na wenzao
wa Sirari kumsaka mtuhumiwa kujibu tuhuma. Polisi wa Sirari wamekiri
kupokea taarifa ya mauaji.
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Sokoni Sirari, Benson Makanya alisema waendesha bodaboda
Sirari na Isebania wamekuwa wakitembea na silaha kama visu na kuchangia
uhalifu hapo. Mama mlezi wa Jeremia, mkazi wa Sirari, Moraha Roman
alisikitishwa na kifo chake na kusema alikulia kwao.
Aliiomba
Serikali imfuatilie mtuhumiwa kwa madai mara nyingi akifanya matukio,
hutorokea Mugumu, Serengeti kwa ndugu zake na kurejea baada ya muda.
Mwili wake umehifadhiwa Hospitali ya Ombo Migori ukisubiri ndugu kutoka
Soneka Kisii
0 comments:
Post a Comment